Na Mapuli Kitina Misalaba
Diwani wa kata ya Ngokolo Mhe. Victor Mkwizu ametembelea na kutoa msaada kwa kaya saba(7) ambao nyumba zao zilianguka kutokana na mvua kubwa iliyonyesha Februari mosi Mwaka huu 2024.
Mtendaji wa mtaa wa Mageuzi kata ya Ngokolo Bwana Faraja Kabyemela amesema kaya saba zenye jumla ya watu 49, zimeathirika na mvua hiyo ambayo iliambatana na upepo mkali hali iliyosababisha uharibifu katika baadhi ya kaya.
Diwani wa kata ya Ngokolo Victor Mkwizu ambaye alikuwa safarini wakati tukio hilo likitokea, leo Ijumaa Februari 9 ametembelea kaya hizo na kutoa pole kwa waathirika ambapo amekabidhi Unga wa Mahindi wa Dona na Sabuni.
“Taarifa hii niliipata wakati nipo safarini niliporudi nikasema nije na mimi kujiridhisha na kuona athari zilizojitokeza lakini pia niweze kuwasalimia wahanga wa maafa haya na kuwapa mkono wangu wa pole kwahiyo nimekuja nikiwa na afisa mtendaji wa kata tutawakabidhi Unga kidogo na Sabuni kama mkono wangu wa pole”.
“Poleni sana lakini nitumia nafasi hii kuwaasa wakazi wote wa mitaa ya Ngokolo na mitaa yake yote saba kila kaya iangalie miundombinu ya Nyumba wanayokaa na kuweza kuchukua tahadhari, tahadhari ni pamoja na kuweza kuona sehemu ambazo zinaashiria ubovu ili ziweze kukarabatiwa”.amesema Diwani Mhe.Mkwizu
Baadhi ya wananchi kutoka kwenye kaya zilizoathirika wamemshukuru Diwani wa kata ya Ngokolo kwa kutoa msaada huo.
Post a Comment