" KULIA SIO UDHAIFU, KUTOLIA SIO USHUJAA

KULIA SIO UDHAIFU, KUTOLIA SIO USHUJAA

 

9a9bbfebbcca73362417de697f341398--positive-vibes-quotes-black-women-art.jpg

Huwa inaumiza sana. Huenda ilikuwa kupitia ujumbe mfupi wa maandishi ama alimtuma rafiki yake kipenzi aje akupe hii taarifa au labda kwa kinywa chake pasipo kujali hisia zako hata kidogo akakuchana kuwa “hakutaki tena.” Masikini ukaachwa pasipo hata kupewa nafasi ya kujieleza wala kujitetea. 

Ukahukumiwa hali ya kuwa hujui kosa lako ni lipi, ukaachwa na yule uliyempenda kwa dhati ya moyo wako na bado unamuhitaji. Unajaribu kutafakari kwa kina lakini hupati jibu, unampigia simu ila haipokelewi, sms zako hazijiwi na kinachokuumiza zaidi sio kuachwa bali ni ule muda ulioutumia pamoja naye. Kwanini hajaheshimu hisia zako?


Ahadi zote zile, mipango yote ile, kila ulichofanya juu yake kimehitimishwa na neno moja kutoka kwake, “Sikutaki tena!” Unaumia ila hakuna unaloweza kufanya kubadili msimamo wake, maana hauna mvuto tena mbele ya macho yake. Huna thamani kwake, huna lolote la kumfanya akusikilize! Inakuuma ila huwezi kubadili msimamo wake. Huo ndio ukweli.

Wengi wamekuwa wahanga wa jambo hili ila wamehifadhi maumivu yao ndani ya nafsi zao. Japo macho yao ni makavu na sura zao zimesheheni furaha ila mioyo yao inabubujika machozi ya damu. Vifua vayo vimehifadhi maumivu yasiyoweza kuelezeka. Mapenzi ni nadharia tete ambayo hata mbele ya fikra za wasomi bado haijaeleweka vyema.

Kila mtu huwa na namna yake ya kukabili hizi hisia. Wengine hunywa pombe, wengine huvuta sigara, wengine huamua kuwa malaya, ambao hushindwa kabisa kuhimili hali zao huwa vichaa, wengine hutukana tu bila sababu, wengine huamua kuapa kuwa hawatopenda tena na wengine hujitoa uhai na huku wengine wakibaki na mfadhaiko kwa muda mrefu yaani wanakufa taratibu.
Huwa unakabiliana vipi dhidi ya msongo wa mawazo?

Kwanza lazima ujue ni sawa kutojihisi sawa. Maumivu unayoyapata ni ushahidi tu kuwa bado unaishi na una nafasi ya kusonga mbele. Bahati mbaya tumelelewa katika kazingira ambayo tumeaminishwa kuwa furaha ndio maisha hivyo tunapaswa kuwa na furaha kila wakati. Tunasahau kuwa maisha ni kama shilingi, umewahi kuona shilingi yenye upande mmoja? Bila shaka jibu ni hapana. Hii ina maana unapoiona furaha basi huo ni upande mmoja tu wa shilingi na upande wa pili ni huzuni.

Unapoumizwa unapaswa kukubali kuwa umeumia, inapunguza mapambano yasiyo na ulazima dhidi ya nafsi yako mwenyewe pia inakusaidia kujipa muda wa kutafakari tiba sahihi ya maumivu hayo. Kutokubali kuwa umeumia huwa inazalisha sumu ndani yako, ukijihisi unataka kulia basi lia sana, lia mno maana inasaidia kuondoa sumu ila tu usilie mbele ya mbaya wako maana hiyo ni kumpa ushindi wa mezani. Jifungie sehemu halafu lia sana kwa faida ya afya yako.

Tafuta watu wa karibu yako kisha zungumza nao kuhusu hali yako, hii pia inasaida kusafisha mtima wako. Tafiti zinaonyesha kuwa watu wengu hufikia maamuzi ya kujiua sababu ya kukosa watu wa kuzungumza nao. Tambua nafasi yako katika kufanya maamuzi yako maana ikiwa utafanya maamuzi mabaya au mazuri wa kwanza kuathiriwa na hayo maamuzi ni wewe. Unatakiwa kuwa na fikra chanya, usiruhusu hisia zikafunika uwezo wako wa kufikiri, wewe ni wewe na sio mwingine yeyote.

Unapoingia kwenye mahusiano lazima utambue huyo mpenzi wako ni binaadamu sio malaika. Chochote kinaweza kutokea wakati wowote usiwe na matarajio makubwa sana yasiyo na uhalisia, utakuja kujutia. Sio kila siku mtakuwa mnakimbizana kwenye bustani za maua na kupulizia mahaba yenye utamu wa asalio kumbuka kuna nyakati ngumu pia umejiandaajke?

Unapoumizwa usijivishe sura ya furaha wakati moyo wako unatokota, inaongeza maumivu. Usiigize maisha kiasi cha kujifanyia maigizo hadi wewe mwenyewe, tambua kuwa umeumia kisha anza kupambana na hali yako katika njia sahihi. Wengine hutumia pombe maana huwafanya wajihisi wapo okay, wengine huvuta madawa ya kulevya kisha hujihisi na wengine hufanya mambo mengie ya hovyo na kujihisi wapo sawa ila ukweli ni kwamba huwa wanajiingiza kaburini mdogo mdogo.

Yangu ni hayo tu. Usivae sura ya furaha hali ya kuwa moyoni una vidonda usipoangalia utavunda ndani hali ya kuwa usoni unatabasamu.

Post a Comment

Previous Post Next Post