" WAJASIRIAMALI 30 WANAOTENGENEZA WAPIGWA MSASA NA SHIRIKA LA TYC SHINYANGA

WAJASIRIAMALI 30 WANAOTENGENEZA WAPIGWA MSASA NA SHIRIKA LA TYC SHINYANGA


v Wafurahia mbinu mpya zinazopunguza gharama za uzalishaji,Watakiwa kutumia vyema Mitandao ya Kijamii kunadi biashara zao,TDT likitia mkono na kufadhili mafunzo hayo

Na,Ibrahim Mwakyoma

Vijana nchini wametakiwa kuitumia vizuri mitandao ya kijamii kama sehemu ya kutangaza na kukuza biashara zao badala ya kuitumia kama sehemu ya masuala ya burudani pekee kama ambavyo baadhi yao wamekuwa wakiitumia.

Rai hiyo imetolewa na Afisa Maendeleo  Manispaa ya Shinyanga Bi.Nyanjula Kiyenze Machi 28,2024 wakati akizungumza katika kilele cha siku mbili za mafunzo kwa wasichana chanuo 30 walionufaika na mafunzo ya ya kuwajengea uwezo katika utengenezaji wa bidhaa za sabuni kwa lengo la kuondoa changamoto mbalimbali zinazowakabili katika uzalishaji wa bidhaa zao yaliyofanyika kati ya Machi 27-28 na kuwataka kudumisha na kuendeleza vikundi kwaajili ya kusaidiana.

“Mafunzo kama haya yanaleta tija kwa vijana,hii inasaidia sana vijana kujiamini,kujitambua na kuweza kujitegemea ili kukuza uchumi wao hivyo mafunzo yanavyofanyika tunawakumbusha vijana kwamba wanapaswa kujitegemea na kutokuwa tegemezi hasa vijana wa kike”amesema Bi.Nyanjula

Aidha amelishukuru Shirika la (TYC) kwa kuendesha mafunzo hayo yaliyowalenga wajasiriamali ambao tayari wanatengeneza bidhaa na hivyo kueleza kwamba yatawasaidia kuongeza thamani katika bidhaa zao ili ziweze kutambulika katika maeneo mbalimbali nchini na kueleza kwamba matarajio ya serikali ni kuwa watawasaidia vijana wengine ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.

“Nawashauri pia vijana watengeneze vikundi vyao,katika vikundi vikundi wanasaidiana na kuinuana,tunategemea vijana kama hawa wakiwa na vikundi wataweza kuendeleza vikundi vyao kwa  kusaidiana kutafuta masoko na sio tu kutegemea mikopo ya asilimia 10% au mikopo ya benki,wao watakapoendelea ndio wataweza kutafuta mitaji zaidi ya biashara zao,wasikae chini,wapambane ili tutakapofika hatua ya kussuport tukute wamepiga hatua”ameongeza Bi.Nyanjula.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Tanzanian Youth and Children (TYC) Bw.Lucas Maganga lililoendesha mafunzo hayo ya bure kwa ufadhili Shirika la Tanzania Development Trust(TDT) ameeleza kwamba yamefanyika kwa lengo la kuimarisha biashara za wajasiriamali wanaojihusisha na utengenezaji wa sabuni  ili kuongeza tija katika maeneo ya utengenezaji,ufungaji na utafutaji wa masoko ya bidhaa wanazozalisha na kubainisha matarajio yaliyopo baada ya mafunzo kukamilika.

“Tumeamua kuendesha mafunzo haya kwasababu tunao watu ambao ni wanufaika wa mradi wa ‘Soap Making Project’ kwa ufadhili wa Shirika la Tanzania Development Trust(TDT) ambao unatelelezwa hapa manispaa na tumedhamiria kuendesha mafunzo haya ili kuimarisha biashara zao,ufungashaji na namna ya kuendesha biashara na sisi tumegundua ya kwamba ni lazima tuhuishe mafunzo yao na wafundishwe namna ya kufanya biashara kwa ubora zaidi kwenye mitaa na hata nje ya mkoa wa Shinyanga”amesema Bw.Maganga

Elizabeth William,Neema Mathias Chidama na Grace Bitekeye ni baadhi ya wajasiriamali walionufaika na mafunzo hayo wameeleza kwamba wamefanikiwa kujifunza mbinu mpya za uzalishaji wa bidhaa zao zinazopunguza gharama za uzalishaji bila kuathiri viwango vya ubora wa bidhaa wanazazozalisha ambazo ni pamoja na fomula mpya za utengenezaji wa sabuni za maji na kutumia fursa hiyo kuwataka wasichana kuepuka tabia ya utegemezi na badala yake wajishughulishe na ujasiriamali.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post