" ASKOFU SANGU AWAALIKA WAKRISTO WOTE KUTAMBUA UKUU WA EKARISTI TAKATIFU

ASKOFU SANGU AWAALIKA WAKRISTO WOTE KUTAMBUA UKUU WA EKARISTI TAKATIFU

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, ametumia mahubiri yake katika Misa ya Alhamisi kuu kuelezea juu ya ukuu wa Sakramenti ya Ekaristi takatifu ndani ya Kanisa.

Askofu Sangu amefafanua kuwa, Kanisa Katoliki linapoadhimisha kumbukumbu ya kuanzishwa kwa Sakramenti ya Ekaristi takatifu (Mwili na damu ya Yesu kristo) kupitia siku ya Alhamisi kuu, linaenzi jambo la pekee ambalo Yesu mwenyewe aliwaachia mitume wake kupitia maumbo ya mkate na divai.

Askofu Sangu ameendelea kuwahakikishia waamini kuwa, nguvu ya Kanisa Katoliki inatokana na kumpokea Yesu Kristo mwenyewe ambaye anashuka kwa wanadamu ambapo yeye mwenyewe aliwapa uwezo mitume wake wa kumshusha kupitia maumbo ya mkate na divai wakati akila nao karamu ya mwisho, kabla ya kukamatwa, kuteswa na kufa Msalabani.

Amesema Kanisa limeendelea na utaratibu wa kumshusha Yesu katika maumbo ya mkate na divai kupitia wandamizi wa mitume ambao ni Maaskofu na Mapadre na kwamba, Ekaristi takatifu inapaswa kuwa msingi wa Imani kwa wakatoliki wote.

Askofu Sangu amewaalika Wakatoliki wote kutambua ukuu wa Ekaristi takatifu na kupitia maadhimisho ya Alhamisi kuu waamushe upya Imani ya uwepo wa Yesu Kristo katika maumbo ya mkate na divai kwa kuhakikisha wanaienzi, wanaipokee, wanaiishi na kuhudhuria Misa takatifu mara kwa mara.

Hali kadhalika amewasisitiza kushiriki Sakramenti ya kitubio kila wakati, ili waonje huruma ya Mungu kwa kusafishwa dhambi zao.

Askofu Sangu pia ametumia nafasi hiyo kuwataka Wakatoliki wote kuwa na upendo kwa wengine, kuacha ubinafsi, kujali shida za wengine, kutendeana wema na kusameheana pale wanapokoseana.

Amewakumbusha waamini wa Jimbo la Shinyanga kuendelea kuwaombea Mashemasi 11 wa Jimbo ambao wanatarajia kupewa Daraja takatifu la Upadre mnamo mwezi Julai mwaka huu, ili Mungu awaimarishe katika safari yao ya wito.

Leo, Kanisa Katoliki kote ulimwenguni linaadhimisha siku ya Alhamisi kuu, ambayo ni kumbukumbu ya Yesu Kristo kuweka Sakramenti ya Ekaristi takatifu, kuanzishwa kwa Sakramenti ya Daraja la Upadre, na kuwekwa kwa amri kuu ya mapendo.

 Pia siku hiyo, Yesu Kristo aliwaosha miguu wanafunzi wake na kula nao karamu ya mwisho kabla ya kukamatwa, kuteswa na kufa msalabani na baadaye siku ya tatu akafufuka.

Wanakwaya wakiimba kwenye Misa ya Alhamisi kuu

Maandamano ya Askofu, Padre, Shemasi, Frateri na watumikiaji kuingia Kanisani

Askofu Sangu akiwa kwenye maandamano ya kuingia Kanisani huku akiwabariki waamini

Misa inaendelea

Sophia Makao akisoma somo la kwanza

Silas Madereke akisoma somo la Pili

Shemasi James Chingila akisoma somo la Injili

Askofu Sangu akitoa homilia

Askofu Sangu akiwaosha miguu waamini ambao wameandaliwa ikiwa ishara ya Yesu alipowaosha miguu wanafunzi wake

Waoshwa miguu

Walelewa wa Shirika la Kijimbo la Maria Mtakatifu Mama wa huruma wakiwa kwenye Misa ya Alhamisi kuu

Watawa wakiwa kwenye Misa ya Alhamisi kuu

Waamini wakiwa kwenye Misa ya Alhamisi kuu

Askofu sangu akipokea matoleo

Waamini wakikomunika

Askofu Sangu akiongoza Ibada ya kuabudu Ekaristi takatifu

 

Post a Comment

Previous Post Next Post