" AZZA HILLAL HAMAD AAHIDI KUSHUGHULIKIA CHANGAMOTO ZA WANANCHI JIMBO LA ITWANGI

AZZA HILLAL HAMAD AAHIDI KUSHUGHULIKIA CHANGAMOTO ZA WANANCHI JIMBO LA ITWANGI


Mgombea wa nafasi ya Ubunge wa Jimbo jipya la Itwangi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Azza Hillal Hamad, ameahidi kushughulikia kwa haraka changamoto zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo, ikiwemo upatikanaji wa maji safi na barabara bora, pindi atakapopewa ridhaa ya kuwa Mbunge baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Akizungumza wakati wa mkutano wa kufunga kampeni uliofanyika leo Oktoba 27, 2025, katika Kata ya Tinde, Azza amesema amedhamiria kuwatumikia wananchi wa Itwangi kwa vitendo na kuhakikisha kila kijiji kinapata huduma muhimu za maendeleo.

“Wananchi wa Itwangi, kabla hata hamjanipigia kura tayari najua matatizo yenu. Oktoba 29 nipigieni kura nyingi za ushindi ili nipate nafasi ya kuwasemea na kuyatatua,” alisema Azza.

Amesema tayari serikali inatekeleza miradi mbalimbali kupitia Ilani ya CCM, ikiwemo ujenzi wa barabara, madaraja na makavati, pamoja na kuboreshwa kwa huduma za maji na afya. Aidha, ameahidi kupigania mradi wa maji wa Tinde Package unaolenga kufikisha huduma ya maji kwa vijiji 18, ili kupunguza adha ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wa Itwangi.

Akieleza mafanikio yaliyopatikana chini ya Serikali ya Awamu ya Sita, Azza ametaja upatikanaji wa umeme katika vijiji vyote 58 vya jimbo hilo, kukamilika kwa maboma ya zahanati, na kuboresha miundombinu ya elimu, akisisitiza kuwa maendeleo hayo ni ushahidi wa kazi nzuri ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Mama Samia ni jasiri, mnyenyekevu na mwenye mapenzi makubwa kwa wananchi. Ametekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, hivyo anapaswa kupewa kura nyingi ili aendelee kuongoza nchi yetu,” alisema Azza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mabala Mlolwa, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo, alimpongeza Azza kwa moyo wake wa kujitolea na uongozi wenye kuzingatia maslahi ya wananchi.

“Azza ni kiongozi mchapakazi na mwenye kujali wananchi wake. Tumpatie kura nyingi ili awe Mbunge wetu wa kwanza wa Jimbo la Itwangi na alete maendeleo zaidi,” alisema Mlolwa.

Mlolwa pia amewaomba wananchi kumpa kura nyingi Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisema uongozi wake umeleta mageuzi makubwa ya maendeleo nchini, na kuwataka wakazi wa Itwangi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 kupiga kura kwa wagombea wote wa CCM kuanzia ngazi ya Udiwani, Ubunge hadi Urais.

Mgombea Ubunge Jimbo la Itwangi kupitia CCM Azza Hillal Hamad akinadi sera kwa wananchi wa Itwangi.






Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, akimuombea kura Mgombea Ubunge wa Jimbo jipya la Itwangi, Mhe. Azza Hillal Hamad.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, akielezea kwa wananchi namna sahihi ya kuwapigia kura wagombea wa CCM katika mkutano wa kufunga kampeni uliofanyika Kata ya Tinde, Oktoba 27, 2025.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa (kulia) akielezea kwa wananchi namna sahihi ya kuwapigia kura wagombea wa CCM katika mkutano wa kufunga kampeni uliofanyika Kata ya Tinde, Oktoba 27, 2025.
Mgombea Ubunge Jimbo la Itwangi kupitia CCM Azza Hillal Hamad akinadi sera kwa wananchi wa Itwangi.
Mgombea Ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo jipya la Itwangi, Mhe. Azza Hillal Hamad, akizungumza na maelfu ya wananchi katika mkutano wa kufunga kampeni uliofanyika Kata ya Tinde, Oktoba 27, 2025, ambapo aliwaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura Oktoba 29.
Mgombea Ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo jipya la Itwangi, Mhe. Azza Hillal Hamad, akizungumza na maelfu ya wananchi katika mkutano wa kufunga kampeni uliofanyika Kata ya Tinde, Oktoba 27, 2025.
Mgombea Ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo jipya la Itwangi, Mhe. Azza Hillal Hamad, akiomba kura wakati akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa kufunga kampeni uliofanyika Kata ya Tinde, Oktoba 27, 2025.


Post a Comment

Previous Post Next Post