
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, ametuma salamu za Pasaka kwa waamini na watu wote, ambapo kupitia salamu hizo, amezungumzia mambo muhimu yanayogusa Malezi ya watoto na haki za mtoto wa kiume, maadili kwa vijana, Uchaguzi mkuu na ule wa Serikali za mitaa, Amani ya nchi pamoja na mafundisho ya Imani.
KUHUSU MALEZI NA KUPUUZWA KWA HAKI ZA MTOTO WA KIUME
Askofu Sangu amewataka wazazi pamoja na kutingwa na shughuli za kila siku za kujiingizia kipato kuhakikisha wanawajibika kikamilifu katika malezi ya watoto.
Amewasisitiza kuwa karibu na watoto wao kwa kugawa muda wa kazi zao ili kuwaepusha na wimbi kubwa la mmomonyoko wa maadili linalokuja kwa kasi, ambalo linachangiwa na kukua kwa teknolojia.
Askofu Sangu amewaasa wazazi na walezi wote kuwa karibu zaidi na watoto na hasa wale wa kiume ambao kwa sasa wanakabiliwa na tishio kubwa la ushoga na kwamba, wanahitaji uangalizi wa pekee kutokana na changamoto nyingi zinazowakabili kwa sababu jamii kubwa imewasahau na kuelekeza nguvu nyingi kumpigania mtoto wa kike pekee.
Ameitahadharisha jamii kutopuuza umuhimu wa nafasi ya mzazi katika malezi ya watoto kwani kwa kufanya hivyo, kizazi cha baadaye kitakuwa hakieleweki kutokana na kugubikwa na hali ya giza.
Askofu Sangu ameitaka jamii na wadau wa haki za watoto kuweka mizani sawa katika ulinzi wa watoto, ambapo ameitaja hatua ya kuendeleza kasumba ya kuwekeza nguvu nyingi katika kuwalinda watoto wa kike pekee na kuwaacha nyuma watoto wa kiume ni jambo la hatari.
Ametolea mfano ndoa nyingi kutodumu kwa sasa ni moja ya hali inayochangiwa na haliya ubaguzi katika malezi ya watoto, ambapo jamii kubwa inajikita zaidi kumwandaa mtoto wa kike kuja kuwa Mama bora, lakini inasahau kumwandaa mtoto wa kiume kuja kuwa baba bora na mwema ndani ya familia.
“Hivyo kila mzazi akae karibu na mwanae na hasa wa kiume ambao kwa sasa wanakabiliwa na tishio kubwa la ushoga. Na hapa nisisitize kuwa mtoto wa kiume leo anahitaji uangalizi wa pekee, bila shaka ninyi ni mashahidi kwamba tumekumbwa na wimbi la kubagua watoto bila kujitambua. Nyingi na hata mara nyingine propaganda zisizofaa kwa maadili na mila zetu zimesisitizwa mno kwa mtoto wa kike na kumsahamu mtoto wa kiume, hii ni hatari zaidi. Hivyo niwasihi tujaribu kuweka mizani sawa, sasa waingereza wanasema “too much is harmful”. Msemo huu si bure. Ndoa nyingi kwa sasa hazidumu, inawezekana ni kwa sababu tumemwandaa zaidi mtoto wa kike kuwa Mama, tukasahamu kuweka mkazo kwa mtoto wa kiume kumwandaa kuwa Baba Mwema”
Askofu Sangu pia amewaasa wazazi na hasa wenye uwezo wa kiuchumi kutoamini matunzo na malezi wanayoyapata watoto wao kwenye shule za gharama kubwa ambako wanawapeleka, na badala yake wanapaswa kutambua kuwa, wao kama wazazi kwa nafasi yao wana wajibu mkubwa kuchangia malezi ya watoto wao ambayo yatawajengea msingi imara wa makuzi ikiwemo kuwarithisha mila nzuri.
KUHUSU MAADILI KWA VIJANA
Askofu Sangu amebainisha kuwa, jamii inapaswa kujiuliza chanzo na chimbuko la hali ya mmomonyoko mkubwa wa maadili kwa vijana ambayo inalalamikiwa na jamii ikiwemo wazazi wenmyewe na kutafuta mwarobaini wa hali hiyo, ambayo haipaswi kufumbiwa macho.
Amemtaka kila mmoja kwa nafasi yake kuwajibika ili kuwa na taifa lenye kizazi kinachoishi kwa kumpendeza Mungu na maadili yanayokubalika kwa wanadamu na kwamba, mmonyoko wa maadili kwa vijana unaoshuhudiwa hivi leo unachangiwa kwa kiasi kikubwa na hali ya kuwepo kwa wazazi wasiowajibika kikamilifu katika malezi na makuzi ya watoto wao, hatua ambayo imesababisha kuwa na kizazi kisichokuwa tayari hata kukabiliana na hali ya changamoto ili kujipatia ushindi, na badala yake kinaamini katika kupata utajiri na mafanikio kwa njia ya mkato bila kufanya kazi.
Ameitaka jamii kushtushwa na hali hiyo ambayo imechochea kwa kiasi kikubwa wimbi la vijana kushinda kwenye vijiwe wakitegemea michezo ya kubahatisha (kubeti) na kucheza Pull ili kuendesha maisha yao ya kila siku na kwamba, vijana wanapaswa kujengwa katika kufanya kazi halali ambazo zitawatoa jasho ili kuleta ufanisi katika maisha yao, familia zao na taifa kwa ujumla.
“Kutokana na kuwa wazazi wasio wajibika, tumefikia hatua ya kuwa na kizazi kisichokuwa tayari kukabiliana na mateso ili kujipatia ushindi. Kizazi ambacho kwa mfano kila mmoja anatafuta mwanya wa kupata utajiri bila hata ya kufanya kazi. Kizazi ambacho mtu yuko tayari kushinda kijiweni akicheza pull kwa kutegemea kupata mahitaji yake kwenye meza hiyo, na wala hakuna hata mmoja anayeshtuka, jamii inaona kama ni kitu cha kawaida tu na cha kimaendeleo, mwingine anatumaini kujipatia kitita cha fedha kwa kucheza michezo ya bahati na sibu, na yuko tayari kutumia gharama kubwa kwa michezo hii ali maarufu “kubeti”, ili kuendesha maisha yake na kuandaa maisha ya kizazi chake kwa njia hiyo. “Jamii iko kimya na mara nyingine hata kushangilia na kupongeza”
KUHUSU UCHAGUZI
Askofu Sangu amewakumbusha watanzania ikiwemo waamini wa dini zote kuendelea kuliombea taifa hasa linapoingia katika kipindi cha uchaguzi wa Wenyeviti wa vijiji, vitongoji na mitaa baadaye mwaka huu pamoja na uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika mwaka kesho 2025, ili chaguzi hizo zifanyike kwa haki, uhuru na Amani .
Askofu Sangu amewakumbusha watanzania kuwa makini na watu wasilolitakia mema taifa wanaotumia kipindi cha uchaguzi kuchochea migogoro ndani ya jamii kwa sababu ya uchu wa madaraka na maslahi yao binafsi , hali ambayo imesababisha baadhi ya mataifa ya Afrika kuingia kwenye machafuko.
Amewataka watanzania wote kutokubali kuwachagua watu wanaotumia ushawishi wa rushwa za aina mbalimbali ili wapate madaraka kwa kuwa watu hao ni hatari kwa ustawi wa taifa na endapo watafanikiwa kuwa viongozi huangalia zaidi maslahi yao binafsi badala ya maslahi ya wengi na kwamba, mtu anayemchagua kiongozi kwa sababu ya kupewa rushwa/hongo anatenda dhambi kubwa na ni mtu hatari asiyekuwa na uchungu na taifa.
Askofu Sangu ametumia nafasi hiyo kuzitaka mamlaka za nchi kutoshiriki kwa namna yoyote kwenye vitendo vinavyomchukiza Mwenyezi Mungu wakati wa uchaguzi na badala yake zitende haki huku zikitambua kuwa, Amani ni tunda la haki na wala si vinginevyo.
Amewasihi viongozi waliopo madarakani kuwa na hekima ya kimungu na wazingatie misingi ya haki na kuepuka vitendo vya upendeleo na ubaguzi kwa wagombea wasiokuwa wa upande wao.
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga ametakwa wananchi waachwe waamue wenyewe ni kiongozi gani wanayemtaka ili kuimarisha hali ya demakrasia yenye kujali misingi ya haki, utu na utengamano wa taifa, kwa kuwa viongozi wanaopatikana kwa wananchi kulazimishwa bila matakwa yao uwajibikaji wao hauna tija kwa taifa na badala yake hufanya juhudi kubwa kujinufaisha wao wenyewe na kuwafurahisha wachache waliowaweka kwenye nafasi hizo.
“Napenda kuwaasa mamlaka zinazohusika, kutoshiriki kwa namna yoyote katika vitendo hivyo vinavyomchukiza Mwenyezi Mungu. Mamlaka husika pia zitende haki. Hapa nasisitiza kuwa Amani daima ni tunda la Haki, na si vinginevyo, Vingozi wetu waliopo madarakani ni lazima wawe na hekima ya Kimungu, wazingatie misingi ya haki na kuepuka vitendo vya upendeleo na ubaguzi kwa wagombea wasiokuwa wa upande wao ili kulivusha taifa katika kipindi hiki cha uchaguzi, Wananchi wanapaswa kuachwa waamue wenyewe ni kiongozi gani wanayemtaka, ili kuimarisha hali ya kidemokrasia yenye kujali misingi ya haki, utu na utengamano wa kitaifa”
Askofu Sangu amewasisitiza Watanzania wote ikiwemo Wakristo na hasa wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika chaguzi zote zinazokuja.
KUHUSU AMANI YA NCHI
Askofu Sangu ametoa wito kwa Wakatoliki wote kuendelea kumwomba Mama Bikra Maria ambaye ni malkia wa Amani na msimamizi wa taifa la Tanzania kwa Imani ya Kanisa Katoliki, ili kwa maombezi yake Tanzania iendelee kuwa na Amani na utulivu.
“Nawaomba Wakristo Wakatoliki tuendelee kumwomba Mama Bikra Maria ambaye ni Malkia wa Amani na msimamizi wa Taifa letu la Tanzania atumombee kwa mwenyezi Mungu ili nchi yetu iendelee kuwa na Amani, umoja na mshikamano”
KUHUSU MAFUNDISHO YA IMANI
Askofu Sangu amewataka Wakristo na hasa Wakatoliki kuwa makini na manabii wa uongo, ambao wanajitafutia utukufu wao wenyewe badala ya Mungu kwa kuwarubuni watu kwa miujiza ili wapate mafanikio ya harakaharaka bila kufanya kazi, badala ya kuwafundisha watu kuhusu kumjua Mungu na hatimae waende kwake mbinguni.
Amesema kwa sababu ya kutosikiliza sauti zilizo sahihi kama Musa alivyomsikiliza Mungu kumeibuka wahubiri wanaopotosha ukweli wa Injili wakifundisha upatikanaji wa maisha ya mbinguni bila jasho wala mateso.
Amewaalika Wakristo kuifahamu vyema nguvu ya roho Mtakatifu ili wawe thabiti katika Imani yao, badala ya kuvutwa na miluzi mingi inayosikika kila kona.
“Kumbe, nawaalika waamini tulifahamu hili, na tutaufahamu ukweli huu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu na si kwa kupitia miluzi mingi inayosikika sasa kila kona. Niwaase kila mmoja wetu kufanya bidii kujua mafundisho ya imani ya kweli kama Mamlaka Fundishi ya Kanisa inavyotuelekeza. “JIHADHARINI NA MANABII WA UONGO, Tusikubali kuyumbishwa na manabii wa uongo wanaolitumia jina la Kristo na shida za watu kujinufaisha wao binafsi huku wakiacha mafundisho ya kweli ya kuwapeleka watu kwa Mungu, badala yake wanafundisha na kurubuni watu kuwa wanaweza kuwafanya matajiri na kuwapa fahari kwa ajili ya maisha ya ulimwengi huu unaopita”
Askofu Sangu amewakumbusha wakristo kuendelea kujiweka karibu zaidi na Mungu kwa kuacha maovu, kuendelea kutenda mema na kuwasaidia wenye shida kama walivyofanya kwenye kipindi cha Kwaresma.
PICHA CHINI NI ZA MATUKIO MBALIMBALI YA MISA YA DOMINIKA YA PASAKA AMBAYO ILIFANYIKA KATIKA PAROKIA YA SHINYANGA MJINI NA KUONGOZWA NA ASKOFU WA JIMBO LA SHINYANGA MHASHAMU LIBERATUS SANGU


































































Post a Comment