" MTOTO WA MIAKA 3 ADAIWA KUBAKWA TINDE HALMASHAURI YA WILAYA YA SHINYANGA

MTOTO WA MIAKA 3 ADAIWA KUBAKWA TINDE HALMASHAURI YA WILAYA YA SHINYANGA


Na Mapuli Kitina Misalaba 

Shirika la msaada wa kisheria kwa wanawake na watoto (PACESH) limeahidi kufuatilia hatima ya kesi ya mtoto wa miaka 3 anayedaiwa kubakwa na kijana wa nyumba ya jirani mwenye umri wa miaka 19, huko katika Kijiji cha Jomu kata ya Tinde Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

PACESH imetoa ahadi hiyo kupitia Afisa Sheria  wake Andrew Jeremia Ntinginya,  wakati akizungumza katika kipindi cha Mwanamke na maisha ambacho kinaandaliwa na Redio Faraja kwa kushirikiana na Mfuko wa ruzuku kwa wanawake Tanzania (WFT-T) kwa ajili ya kusaidia mpango wa taifa wa MTAKUWWA, ambao umelenga kutokomeza vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto.

Ntinginya amebainisha kuwa, PACESH itafuatilia hatima ya kesi hiyo katika ofisi ya taifa ya Mashtaka ambayo ina mamlaka ya kisheria ya kusimamia kesi hizo, ili kujua kama imetolewa hukumu bila mlalamikaji kuwepo au hatua nyingine za kisheria zinaendelea, ili waone ni kwa namna gani wanaweza kusaidia. 

Awali mama wa mtoto huyo (42) aliiambia Redio Faraja kuwa, mwanaye aliyekuwa na umri wa miaka 3 wakati huo, alibakwa na kijana wa jirani aliyemtaja kwa Jina moja la James (19) wakati akicheza na wenzake mnamo Februari mwaka jana 2023 .

Alisema baada ya tuko hilo Mama wa mtuhumiwa alikwenda kumshtaki kwa  Diwani wa Kata ya Tinde akidai fidia ya kudhalilishwa, lakini baada ya kutoa maelezo yake na mtoto mwenyewe kueleza walibaini Mama wa mtuhumiwa alikuwa akifanya njama za kutaka kukwepa kesi hiyo.

Hivyo wakashirikiana na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata Tinde pamoja na Jeshi la Polisi mpaka kesi hiyo ikafikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Shinyanga, ambapo mnamo mwezi Julai mwaka jana 2023 na waliitwa kutoa maelezo ya awali, lakini kutoka Julai mwaka jana mpaka sasa hajui kinachoendelea baada ya Mawakili wa Serikali kumwambia asuburi mpaka atakapoitwa kwa ajili ya kuendelea na kesi.

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Tinde Bi. Eva Mlowe, amesema Mama huyo alifika ofisi za Kata akiwa na mwanaye aliyedai kubakwa huku mtoto mwenyewe akimtaja Mtuhumiwa kuwa ndiye alimfanyia kitendo hicho, hatua iliyowalazimu kwenda kuchukua Fomu namba tatu ya Polisi (PF3) na baadaye kumpeleka mtoto huyo katika Kituo cha Afya Tinde kwa ajili ya uchunguzi ambapo Madaktari walithibitisha  kuwa ameingiliwa. 

Amesema baada ya vipimo kukamilika waliipeleka kesi hiyo Polisi kituo cha Tinde ambao nao waliendelea na hatua nyingine za kumkamata Mtuhumiwa pamoja na kuipeleka Mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria lakini mpaka sasa hajui hatima yake.

Redio Faraja pia inaendelea kufuatilia kwenye Ofisi ya Taifa ya Mashtaka mkoa wa Shinyanga ili kujua hatima ya kesi hiyo.

Post a Comment

Previous Post Next Post