" MAJAMBAZI WANNE WAFARIKI KWA RISASI BAADA YA KUFANYA MAUAJI YA MTU MMOJA

MAJAMBAZI WANNE WAFARIKI KWA RISASI BAADA YA KUFANYA MAUAJI YA MTU MMOJA

Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limethibitisha vifo vya majambazi wanne waliouawa kwa kupigwa risasi katika majibizano na askari polisi wakati wa operesheni maalum ya kuwakabili wahalifu waliokuwa wakihusika na matukio ya mauaji na uporaji wa kutumia silaha.

Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, tukio hilo lilitokea wakati askari wakitekeleza majukumu yao ya ulinzi na usalama, ambapo majambazi hao walipambana na askari kwa kutumia silaha za moto. Majambazi hao walipigwa risasi na baadaye walifariki dunia walipokuwa wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi.

Majambazi waliokufa wametajwa kuwa ni Eliuta Mapunda, Abdul Chiba, Justine na Bruce Mwasenga, ambao walikuwa wakitafutwa kwa kuhusika na matukio mbalimbali ya uhalifu katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa na Katavi.

Taarifa ya Polisi inaeleza kuwa majambazi hao walihusishwa na mauaji ya wananchi wasiopungua 30, waliouawa kwa kupigwa risasi katika matukio tofauti ya uporaji na uhalifu wa kutumia silaha.

Katika operesheni hiyo, askari walifanikiwa kukamata mali mbalimbali zinazodhaniwa kuwa za wizi, ikiwemo simu janja 30, simu ndogo 172, mashine ya POS ya Benki ya CRDB, bastola moja, risasi nne, ganda moja la risasi, pamoja na nondo mbili za kuvunjia milango na makufuli.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limesema linaendelea na msako mkali dhidi ya wahalifu wengine, huku likiwataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi kwa kutoa taarifa za uhalifu ili kudumisha amani na usalama.

 

 

Post a Comment

Previous Post Next Post