" MUUMINI AVUNJA UKIMYA: ALITAKA KANISA KATOLIKI KULINDA UMOJA NA HESHIMA

MUUMINI AVUNJA UKIMYA: ALITAKA KANISA KATOLIKI KULINDA UMOJA NA HESHIMA


 Na Mwandishi wetu, Misalaba Media

Muumini wa Kanisa Katoliki nchini, Mwalimu Ludovicky Joseph, ametoa wito kwa viongozi na waumini wa kanisa hilo kuzingatia mazungumzo ya wazi, unyenyekevu wa kiuongozi na kulinda umoja wa Kanisa, kufuatia mjadala unaoendelea kuhusu kauli na mwenendo wa baadhi ya viongozi wa juu wa kanisa hilo.

‎Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 30,2025 Ludovicky amesema ni muhimu kwa Kanisa Katoliki kuendelea kuwa mahali pa amani, haki na kusikilizana, badala ya kuingia katika migawanyiko inayoweza kuligawa Kanisa na kuwaumiza waumini.

‎Amesisitiza kuwa Kanisa Katoliki ni jumuiya ya waamini wote, hivyo uongozi wa kiroho unapaswa kujengwa juu ya misingi ya huduma, unyenyekevu na mafundisho ya Injili. Ameongeza kuwa kuhoji au kuuliza maswali kwa heshima kuhusu masuala ya kanisa si dhambi, bali ni sehemu ya kukua kiimani na kulilinda Kanisa dhidi ya migawanyiko.

‎Vilevile, Ludovicky amesisitiza umuhimu wa matumizi ya lugha ya staha na heshima, hasa katika masuala nyeti yanayogusa imani na jamii kwa ujumla. Amesema madhabahu na majukwaa ya kidini yanapaswa kuwa maeneo ya faraja, mafundisho na maridhiano, si ya maneno makali au lawama.

‎“Viongozi wa kiroho wanapaswa kuwa mfano wa unyenyekevu na upendo, hata wanapokosoa au kusahihisha,” amesema Ludovicky.

‎Aidha, ameeleza kuwa Kanisa lina nafasi muhimu katika kuelimisha jamii kuhusu maadili, haki na ustawi wa jamii, lakini akashauri jukumu hilo litekelezwe kwa busara na bila kuonekana kuegemea upande wa siasa za vyama, kwani Kanisa linapaswa kubaki kuwa sauti ya wote na kiunganishi cha umoja wa Taifa.

‎Ludovicky ameongeza kuwa Kanisa Katoliki lina taratibu zake za ndani za kushughulikia malalamiko na masuala yanayohitaji ufafanuzi, hivyo kufuata taratibu hizo kwa amani na heshima ndiyo njia sahihi ya kulinda taswira na mshikamano wa Kanisa.

‎Amehitimisha kwa kutoa wito wa kutanguliza mazungumzo, kusikilizana na upendo, akieleza imani yake kuwa kwa kufanya hivyo, Kanisa Katoliki litaendelea kuwa imara, lenye mshikamano na linaloongoza jamii kwa mfano mwema

 

Post a Comment

Previous Post Next Post