Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imedhamiria kutatua changamoto ya migongano
baina ya binadamu na wanyamapori huku
ikisisitiza kuwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 imeweka kipaumbele katika kutatua changamoto hiyo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii,
Mhe. Angellah Kairuki (Mb) wakati wa zoezi la kuwarudisha tembo hifadhini
lililofanyika Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya leo Mei 9,2024.
"Tumefanikiwa
kuwarudisha hifadhini tembo takriban 61 na leo tumefukuza tembo 18"
Mhe. Kairuki amesisitiza.
Amesema hiyo inathibitisha umakini wa Serikali ya
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kujali usalama wa maisha ya wananchi
na mali zao na uhifadhi wa
rasilimali za wanyamapori na misitu.
Waziri Kairuki amesisitiza kuwa Serikali itafanya
kila liwezekanalo kutatua changamoto za
wanyamapori wakali na waharibifu nchini hususan
tembo, Simba fisi madoa, chui, mamba,
kiboko, nyani na tumbili.
"Tutaendelea
kuchukua hatua kwa mujibu wa kila aina ya wanyama na mikakati ya wanyama
husika" amesisitiza.
Amesema zoezi
hilo la kufukuza tembo kwa kutumia helikopta limeambatana na kufunga mikanda ya
mawasiliano kwa tembo viongozi wa
makundi mbalimbali ambapo mpaka sasa imeshafungwa mikanda miwili lakini zoezi
litamalizia kwa mkanda wa tatu.
Pia, amesema
Rais Samia ameelekeza kwamba wananchi walioathirika na wanyamapori
wakali na waharibifu walipwe kifuta jasho/machozi
katika vijiji vya
Igunda , Rujewa, Mapogoro, Mlungu, lwalanje,Vikaye, Nyeregete, Manyenga
na Mwanavala.
Aidha, Mhe. Kairuki amezielekeza Taasisi za TANAPA,
TAWA na TFS kuendelea kutoa elimu ya uhifadhi mazingira na namna ya kujikinga
na wanyamapori wakali na waharibifu pindi wanapovamia makazi yao.
Mkutano huo umehudhuriwa na Watendaji, Maafisa
Waandamizi na Viongozi mbalimbali kutoka
Wizara ya Maliasili na Utalii,TAWA, TAWIRI, TANAPA, TFS, viongozi wa Chama pamoja na wananchi.




Post a Comment