Ticker

6/recent/ticker-posts

MADIWANI WA VITI MAALUM HALMASHAURI YA WILAYA YA SHINYANGA WAWASIHI WANAWAKE KUJIEPUSHA NA MIKOPO YENYE RIBA KUBWA (KAUSHA DAMU)

Na Mapuli Kitina Misalaba

Madiwani wa viti maalum Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga wamewasihi wanawake kujiepusha na mikopo yenye riba kubwa (Kausha damu) huku wakiwasisitiza kusubiri mikopo ya serikali inayotolewa bila riba.

Wameyasema hayo leo Julai 13,2024 kwenye ziara yao kata ya Pandagichiza pamoja na kata ya Mwalukwa ambapo ziara hiyo imelenga kuhamasisha wanawake na wanachama wa CCM na jumuiya zake kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura, kuhamasisha wanawake kujitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, Usajili wa wanachama wa CCM na jumuiya zake pamoja na na kukemea Ukatili wa kijinsia.

Madiwani wa viti maalum akiwemo Mwenyekiti wa madiwani viti maalum Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ambaye ni diwani wa viti maalum kata ya Lyabukande Mhe. Zawadi Lufungulo Mwasha pamoja na Katibu wa madiwani  viti maalum Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ambaye pia ni diwani wa viti maalum kata ya Tinde Mhe. Anastazia Robart Njile wamewahimiza wanawake kujiepusha na mikopo yenye riba kubwa.

Wamesema mikopo yenye riba kubwa imekuwa ikisababisha migogoro katika familia ambapo wamesema ili kuwa salama zaidi ni vema kusubiri mikopo ya serikali ambayo inatolewa bila riba kupitia Benki huku wakiwahimiza wanawake kuendelea kusajili vikundi vyao ili kuwa na sifa za kupata mikopo hiyo ya serikali.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ambaye pia ni diwani wa kata ya Mwalukwa Mhe. Ngassa Mboje amesema fedha za mikopo zaidi ya Milioni mia sita zinatarajiwa kutolewa katika makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ambapo amewahimiza wanawake kuimarisha vikundi vyao ili kuwa tayari kupata mikopo baada ya serikali kutoa maelekezo.

Baadhi ya wakazi wa kata ya Pandagichiza pamoja na Mwalukwa wametumia nafasi hiyo kuiomba serikali kuharakisha mikopo hiyo ili kupunguza au kumaliza kabisa migogoro inayotokea katika familia.

Katika hatua nyingine Madiwani wa viti maalum Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungani wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na Mbunge wa jimbo la Solwa Mhe. Ahmed Salum kwa kuendelea kuleta maendeleo katika jimbo hilo  kupitia miradi mbalimbali.

Pia wamempongeza diwani wa kata ya Pandagichiza Mhe. Charles Masele Kabogo pamoja na diwani wa kata ya Mwalukwa Mhe. Ngassa Mboje kwa usimamizi mzuri katika miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika kata zao.

Madiwani wa viti maalum Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga katika ziara yao ya kutembelea mradi wa ujenzi wa madarasa mawili shule ya msingi Shilabela kata ya Pandagichiza leo Julai 13,2024.





 

Post a Comment

0 Comments