Na Moshi Ndugulile
Waziri wa habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye, amesema serikali kupitia mradi wa Tanzania ya kidijitali imetoa zaidi ya Shilingi Bilioni 4.27 kwa Mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya ujenzi wa minara 30 ya mawasiliano,ambapo takribani watu 421,259 waranufaika.
Waziri Nnauye ameeleza kuwa minara hiyo ya mawasiliano ya simu inajengwa kwenye jumla ya kata 29,na vijiji 83 Mkoani Shinyanga kwa lengo la kufikisha huduma ya mawasiliano kwa watu wote yakiwemo maeneo ya pembezoni
Akiwa Mkoani Shinyanga kwa ziara ya siku moja iliyolenga kukagua mradi wa ujenzi wa minara hiyo, Waziri Nape Nnauye amesema serikali imepata fedha kutoka Benki ya dunia kiasi cha Dola za Marekani milioni 150 kwa ajili ya kupeleka miundombinu ya mawasiliano kwa wananchi walioko vijijini.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa mawasiliano kwa wote, UCSAF, Justina Mashiba amesema serikali kupitia kampuni binafsi inajenga jumla ya minara 758 nchini kote.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe Anamringi Macha pamoja na mambo mengine, amesema serikali ya Mkoa wa Shinyanga itahakikisha inawekeza ujenzi wa miundo mbinu ya Barabara itakayorahisisha kuyafikia maeneo inapojengwa minara ya mawasiliano.
Kwa upande wao wabunge Boniphace Butondo wa jimbo la kishapu na Emanuel Cherehani wa jimbo la Ushetu wamepongeza juhudi za serikali kuwekeza kwenye huduma ya mawasiliano kwa wote,ambapo wamesema ujenzi wa minara hiyo itasaidia kuondoa changamoto ya ukosefu wa mawasiliano kwa wananchi.
Waziri Nape akiwa Mkoani Shinyanga ametembelea na kukagua baadhi ya miradi ukiwemo ujenzi wa mnara wa Mawasiliano uliopo kijiji cha Busangwa, wilayani Kishapu na mnara wa mawasiliano uliopo kijiji cha Ngokolo kata ya Nyamilangamo halmashauri ya Ushetu, wilayani Kahama.
---MWISHO---
0 Comments