Na Mapuli Kitina Misalaba
Timu ya Salawe Stars imeibuka washindi wa mashindano
ya Krismas Cup 2024, yaliyomalizika leo Desemba 19, 2024 kwa fainali kali dhidi
ya Beya FC na kwamba ligi hiyo imeandaliwa na Makamba Mussa Lameck kwa lengo la
kuibua vipaji vya michezo.
Katika mchezo huo ambao umechezwa kwa dakika 90 bila
kufungana, Salawe Stars walitawazwa mabingwa baada ya kushinda mikwaju ya penati
5-4, na kujinyakulia kombe pamoja na zawadi ya Shilingi milioni moja.
Mshindi wa pili, Beya FC, wamezoa zawadi ya Shilingi
laki tano, huku Mwasenge FC wakishika nafasi ya tatu na kupata Shilingi laki
mbili.
Wachezaji bora, mfungaji bora, kipa bora, na timu
yenye nidhamu pia walitunukiwa zawadi za fedha, kutambua mchango wao kwenye
mashindano hayo.
Mgeni rasmi wa fainali hizo, Diwani wa Kata ya Salawe, Mhe. Joseph Buyugu,
ameipongeza Salawe Stars kwa ushindi huo na kuwaomba wadau wa michezo kumuiga
Makamba Mussa Lameck ili kuandaa mashindano zaidi.
“Michezo
si tu afya, bali pia ni njia ya kujenga upendo na mshikamano. Nawashauri timu
zilizoshiriki ziendelee kujifunza. Natamani kuona ligi kama hizi zinaendelea
ili kuibua vipaji na kuimarisha michezo wilayani Shinyanga,”
amesema Buyugu.
Mdhamini wa mashindano hayo, Makamba Mussa Lameck, ameipongeza jamii kwa
kujitokeza kwa wingi kushuhudia michezo ambapo amekanusha uvumi kuwa mashindano
hayo yalihusiana na siasa, akisisitiza kuwa lengo lake kuu ni kuibua vipaji vya
michezo kwa vijana.
“Mashindano
haya hayakuhusiana na siasa. Ni jitihada za kuibua vipaji na kuwapa vijana wetu
fursa ya kushiriki mashindano makubwa. Nawahakikishia mashindano haya
yataendelea kila mwaka,” amesema Makamba.
Pamoja na changamoto za kisiasa zilizojaribu
kukwamisha ligi hiyo, Makamba ameishukuru serikali ya kijiji kwa kusimama imara
kuhakikisha mashindano hayo yanafanikiwa.
Kwa mujibu wa msimamizi wa mashindano hayo, Mwalimu
Emmanuel Enock Kijida, vijana 50 kati ya timu 16 zilizoshiriki mashindano hayo
wamechaguliwa kuunda timu moja itakayoshiriki mashindano mbalimbali.
Mashindano ya Krismas Cup 2024 yamedhaminiwa na
Makamba Mussa Lameck kupitia kampuni ya MCL, inayojihusisha na biashara ya
nafaka, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuchochea maendeleo ya michezo mkoani
Shinyanga.
Post a Comment