Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Kanali Ahmed Abbas amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa jumla ya shilingi Bilioni 18 kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), kwa ajili kufanikisha ujenzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Kampasi ya Songea.
Kanali Abbas ametoa pongezi hizo katika hafla ya makabidhiano ya eneo la ujenzi wa IAA Kampasi ya Songea kwa Mkandarasi, Mei 08, 2025 mtaa wa Pambazuko Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
“Ruvuma tunaenda kukamilisha ndoto tuliyokuwa nayo ya muda mrefu ya kupata chuo kikubwa, chuo hiki kitasaidia kuongeza idadi ya wasomi, kitaamsha biashara ndani ya mkoa, pia kitasaidia kukuza huduma za kijamii na kuchochea uwekezaji katika sekta binafsi”, amesema Kanali Abbas.
Aidha, Kanali Abbas ameupongeza Uongozi wa IAA kwa uamuzi wa kizalendo wa kufungua Kampasi mkoani Ruvuma , ambayo itatambulisha mkoa kitaifa na kimataifa na itakuwa chachu ya maendeleo ya elimu na kutoa ajira kwa wananchi.
Naye Mbunge wa Songea Mjini na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Damasi Ndumbaro amesema Serikali imefanya kazi kubwa na itaendelea kuleta maendeleo katika mkoa. Amewataka Wananchi kuendelea kuiunga mkono Serikali katika jitihada za kuleta maendeleo kwa wananchi.
Mkuu wa chuo IAA, Prof.Eliamani Sedoyeka pamoja na kumshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi huo, amewashukuru pia wananchi wa mkoa wa Ruvuma kwa ushirikiano wao wanaouonesha.
Vile vile, Prof. Sedoyeka amesema IAA itajenga jengo lenye hadhi ya kimataifa, huku akibainisha kuwa lengo la IAA ni kuhakikisha kwamba kampasi ya Songea inakuwa kubwa sana katika ukanda wa kusini mwa Tanzania.
Jengo hili litakuwa na ukubwa wa ghorofa tano, uwezo wa kuchukua watu zaidi ya 4500; ndani yake likiwa na madarasa, maktaba, kumbi za mikutano, ofisi na maabara za Kompyuta. Litajengwa kwa muda wa miezi 12 na Mkandarasi China Aero Technology chini ya msimamizi mshauri Y&P Architect (T) Ltd.
Post a Comment