" KONGAMANO LA KITAIFA LA AFYA YA AKILI KUFANYIKA KAHAMA MEI 30 HADI 31, 2025

KONGAMANO LA KITAIFA LA AFYA YA AKILI KUFANYIKA KAHAMA MEI 30 HADI 31, 2025

 

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Yudas Ndungile akizungumza na waandishi wa habari
Na Mwandishi wetu 

Serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo WAYDS Tanzania, imezindua rasmi Kongamano la Kitaifa la Afya ya Akili, litakalofanyika kwa siku mbili mfululizo kuanzia Mei 30 hadi 31, 2025 katika Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga.

Akizungumza na wanahabari wakati wa uzinduzi huo, leo Mei 29,2025 Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Yudas Ndungile, amesema kuwa kongamano hilo ni la kwanza kufanyika katika mkoa wa Shinyanga na linalenga kuimarisha ushirikiano kati ya sekta mbalimbali katika kuboresha huduma za afya ya akili nchini.

“Zaidi ya vijana 300 wenye umri kati ya miaka 18 hadi 35 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania wanatarajiwa kushiriki katika kongamano hili muhimu,”amesema Dkt. Ndungile.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa WAYDS Tanzania, ambaye pia ni mratibu mkuu wa Tanzania Mental Health Summit,  Charles Deogratius, ameeleza kuwa kongamano hilo ni jukwaa mahsusi la kuwakutanisha wadau kutoka sekta zote kwa ajili ya kujadili changamoto zinazokumba afya ya akili nchini na kuibua suluhisho endelevu.

“Tutakuwa na mijadala ya kitaalam, warsha za kielimu na kijamii, zenye lengo la kuongeza uelewa na kuchochea hatua jumuishi katika kutatua changamoto za afya ya akili,” amesisitiza Deogratius.

Kongamano hilo limebebwa na kauli mbiu: “Hatua Shiriki na Jumuishi: Kukuza Ushirikiano Katika Afya ya Akili kwa Maendeleo Endelevu.”

Wadau wa afya, viongozi wa serikali, asasi za kiraia, wanataaluma, na wananchi kwa ujumla wanahimizwa kushiriki kikamilifu katika jukwaa hilo ambalo linaashiria mwelekeo mpya wa kitaifa kuhusu afya ya akili kwa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Mkurugenzi Mtendaji wa WAYDS Tanzania, ambaye pia ni mratibu mkuu wa Tanzania Mental Health Summit, Charles Deogratius, akizungumza
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Yudas Ndungile akizungumza

Post a Comment

Previous Post Next Post