Na Lydia Ezra Lugakila, Misalaba Media
Wafugaji katika wilaya ya Missenyi mkoani Kagera wamepongeza mabadiliko makubwa yaliyofanyika chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza kwa niaba ya wafugaji hao Mwenyekiti wa wafugaji wa wilaya hiyo, Abdul Majid Kayondo, ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kutokana na kuleta maendeleo ambayo yameleta tija kwa wafugaji, jambo ambalo halikuwahi kushuhudiwa hapo awali.
Kayondo amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kata ya Mutukula Wilayani Missenyi mkoani Kagera.
Kayondo amesema kuwa wafugaji wanatambua juhudi za Serikali katika kuboresha sekta ya ufugaji ikiwemo kupatiwa Elimu ya kutosha katika masuala ya kilimo cha kisasa na ufugaji.
"Sisi Kama waislam tunasema mshukuruni mtu akiwa bado yu hai kwakweli Rais Samia anastahili pongezi" alisema Kayondo
Ameongeza kuwa miradi mbalimbali ya maendeleo imeanzishwa katika awamu ya sita huku ushirikiano kati ya wafugaji na serikali ukiimarika.
"kipindi cha nyuma ilikuwa mtu huwezi kumuhitaji waziri mwenye dhamana akakuhitikia kwa haraka lakini kwa sasa Mawaziri tunashauriana na wanatufikia kwa haraka tukiwahitaji" alisema Mwenyekiti huyo.
Pia Kayondo amewakumbusha vijana kujiajiri kupitia kilimo na ufugaji, badala ya kutegemea ajira rasmi.
Afisa Mifugo wa Wilaya, Dr. Edward Aligawesa, ameongeza kuwa sekta ya ufugaji inachangia kwa kiasi kikubwa pato la halmashauri ya wilaya ya Missenyi na kuwataka wafugaji kuwa wazalendo huku akiwahimiza kutumia minada na rasilimali zilizopo kwa faida zaidi.
Kayondo ameahidi kuwapambania vijana kupata maarifa ya ufugaji ambapo amewataka wafugaji kuendelea kuwa mfano bora wa uzalendo na ubunifu katika sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa wilaya na mkoa wa Kagera kwa ujumla.
Post a Comment