Itigi, Singida – Wimbi la hamasa limezidi kushika kasi katika Wilaya ya Itigi, ambapo wananchi pamoja na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameendelea kumhimiza mfanyabiashara maarufu wa matrekta na vifaa vya kilimo, Ndugu Msafiri Ng’ambi maarufu kama Mdau, kuchukua fomu ya kuomba kugombea Ubunge wa Jimbo la Itigi kupitia chama hicho tawala.
Wakizungumza katika mikusanyiko ya kijamii na vikao vya ndani ya chama, wanachama wa CCM wamesisitiza kuwa muda umefika kwa chama kumtazama mtu ambaye ana rekodi ya kusaidia wananchi kwa vitendo, bila kuwa na madaraka yoyote ya kisiasa. Wanadai kuwa Msafiri Ng’ambi ameonyesha dhamira ya kweli ya maendeleo kwa kuchangia zana za kilimo, kusaidia shughuli za kijamii, na kuwa karibu na watu wa makundi yote bila ubaguzi.
“Tunamhitaji mtu anayejua shida za mkulima, mfanyabiashara mdogo na kijana wa Itigi. Mdau ni mtu wetu, anastahili kuliongoza Jimbo letu kupitia CCM,” alisema mmoja wa wazee wa chama wakati wa kikao kilichofanyika Kata ya Itigi Mjini.
Pia vijana na wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika kampeni ya kumshawishi achukue fomu, wakiona katika Msafiri Ng’ambi mfano wa kiongozi mchapakazi, mnyenyekevu na mpenda maendeleo.
“Tunahitaji mbunge ambaye ataibeba Itigi kisiasa na kiuchumi. Hatuwezi tena kujaribu bahati. Tunamwomba Mdau achukue fomu na sisi tutamsaidia kuhakikisha anapita kwenye kura za maoni hadi Bungeni,” alisema mmoja wa viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) katika wilaya hiyo.
Wito huu kutoka kwa wananchi na wanachama wa CCM umeweka wazi kuwa jina la Msafiri Ng’ambi sasa limegeuka kuwa sauti ya matumaini mapya kwa Jimbo la Itigi, huku wengi wakiamini kuwa atakuwa chaguo sahihi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 iwapo atakubali ombi la wananchi na kuchukua fomu ya kugombea kupitia CCM.
Alipopigiwa simu kuzungumzia suala hilo, Msafiri Ng'ambi alisema jambo hilo la kugombea Ubunge hajawahi kulifikiria na kwamba katika kufanya kazi kwake au kusaidia jamii lengo lake kuu ni kuhakikisha maendeleo yanaendelee kukua katika hali ya kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Tanzania.
Post a Comment