Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Janeth Magomi.
Maria Raulent akizungumza kwa niaba ya familia ya marehemu.
Na Mapuli Kitina Misalaba
Familia ya Daniel Masanja mkazi wa Tambukareli,
Manispaa ya Shinyanga, imeliomba Jeshi la Polisi kuongeza juhudi katika
kumtafuta mtuhumiwa anayedaiwa kumuua kwa kumchoma kisu kijana wao, Bernardo
Masanja, ili hatua za kisheria zichukuliwe na haki ipatikane.
Akizungumza kwa niaba
ya familia hiyo, Maria Raulent amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo
Juni 22, 2025, ambapo marehemu Bernardo alikutwa amefariki dunia kwa kuchomwa
na kitu chenye ncha kali sehemu ya kifua akiwa eneo la karibu na kituo cha biashara
ya bodaboda alikokuwa akifanya shughuli zake.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Mtaa wa Tambukareli, Bi. Tabitha Shilingi, amewataka wananchi
kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake kuwasilisha migogoro yao kwa
viongozi wa serikali au taasisi za dini kwa ajili ya suluhu.
Akizungumza na Misalaba Media, Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Janeth Magomi,
amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa Jeshi la Polisi
linaendelea na msako mkali dhidi ya mtuhumiwa.
“Kwanza napenda
kuthibitisha kuwa tukio hili limeripotiwa rasmi ofisini kwangu tarehe 22 Juni 2025,
majira ya saa sita usiku. Marehemu alifahamika kwa jina la Belenado Masanja,
mwenye umri wa miaka 24, mkazi wa Tambukareli, ambaye alikutwa amechomwa kisu
sehemu ya kifua upande wa kushoto,” amesema SACP Magomi.
Ameongeza kuwa
mtuhumiwa anayefahamika kwa jina moja la Kulwa
alihusika katika ugomvi wa kugombea abiria na marehemu, ambapo wote wawili
walikuwa waendesha bodaboda. Jeshi la Polisi limeanza uchunguzi wa kina na
msako mkali unaendelea huku SACP Magomi.
Mwili wa marehemu
umehifadhiwa katika Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga na kwamba mazishi yanatarajiwa
kufanyika Jumanne wiki ijayo.
Post a Comment