Na Mapuli Kitina Misalaba
Mwanamke jasiri na mwenye ulemavu, Mwajuma K. Mbogo, leo Juni
29, 2025, ameandika historia mpya kwa kujitokeza kuchukua fomu
ya kuwania nafasi ya udiwani katika Kata ya
Ngokolo, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Uamuzi wake umetokana
na msukumo alioupata baada ya kusikiliza hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan,
alipozungumza kwa msisitizo juu ya usawa, ushiriki wa wanawake na watu wenye
ulemavu katika uongozi, wakati wa kufunga Bunge la Jamhuri hivi karibuni.
"Hotuba ya
Mheshimiwa Rais Samia imenigusa sana. Nimeamua kusimama ili niwe sauti ya walio
kimya, hasa wanawake na watu wenye ulemavu. Tunaweza, tukipewa nafasi,"
amesema Mwajuma mara baada ya kuchukua fomu.
Mwajuma amesema ana uzoefu mkubwa wa kiuongozi, akitaja nyadhifa mbalimbali
alizowahi kushika ikiwemo kuwa Mjumbe wa Kamati ya Ustawi
wa Jamii, Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Wazazi Tawi la Mwadui mwaka 2015, Mjumbe
wa Kamati ya Utekelezaji ya UWT tawi la Mwadui, na kwa sasa ni Mwenyekiti Msaidizi wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Viungo Tanzania
(CHAWATA) Wilaya ya Shinyanga, sambamba na kuwa Mjumbe wa SHIVYAWATA Wilaya ya Shinyanga Mjini.
Ameeleza kuwa licha ya
changamoto alizopitia, ikiwemo kupingwa na baadhi ya watu kwa sababu ya hali
yake ya ulemavu wakati wa uchaguzi wa jumuiya ya wazazi, hajawahi kukata tamaa
na sasa anaamini ni muda wake wa kusimama kwa ajili ya kuwatumikia wananchi.
"Wakati
mwingine unakataliwa si kwa sababu huna uwezo, bali kwa sababu tu ya hali yako.
Lakini mimi naamini katika uwezo wa mtu, si kizuizi cha mwili,"
ameongeza kwa msisitizo.
Zoezi la uchukuaji fomu
za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi
linaendelea kote nchini, kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.


Post a Comment