Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imethibitisha kuipatia Klabu ya Simba Sports Club ruhusa rasmi ya kufanya mazoezi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, siku ya Jumamosi, tarehe 14 Juni 2025. Ridhia hiyo imetolewa kufuatia ombi rasmi la klabu hiyo lililotumwa kupitia barua yenye Kumbukumbu Na. SSC/WUSM/09/06/2025/01.
Katika barua yake kwa Simba SC, wizara imeeleza kuwa haina pingamizi lolote kwa timu hiyo kufanya mazoezi rasmi kwenye uwanja huo, ikiwa ni maandalizi ya mchezo namba 184 wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Wizara imebainisha kuwa uwanja huo, pamoja na viwanja vingine vya serikali, unapatikana kwa matumizi ya vilabu vyote vinavyoshiriki ligi kwa usawa na bila upendeleo wowote.
Aidha, wizara imesisitiza kuwa maamuzi yake yanalenga kuhakikisha haki na usawa vinazingatiwa kwa vilabu vyote, na kwamba hakuna sababu ya kuzuia Simba SC kutumia uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya maandalizi ya mechi hiyo muhimu.
Wakati huo huo, klabu hiyo imekumbushwa kuhakikisha inakamilisha taratibu zote muhimu za maandalizi ya mechi, ikiwemo kuhudhuria mkutano wa maandalizi wa kabla ya mechi (pre-match meeting), unaoratibiwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania.
Post a Comment