" TAASISI ZA UMMA ZATAKIWA KUTENGA ASILIMIA 30 YA ZABUNI INAZOTANGAZA KWA MAKUNDI MAALUM

TAASISI ZA UMMA ZATAKIWA KUTENGA ASILIMIA 30 YA ZABUNI INAZOTANGAZA KWA MAKUNDI MAALUM

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt.Dorothy Gwajima, akizungumza.

Na Seif Mangwangi, Arusha

SERIKALI imezitaka Taasisi za umma   kutenga asilimia 30 ya zabuni inazozifanya kwa kila mwaka na kuzitoa  kwa kampuni za wazawa ikiwemo makundi maalum ya walemavu, wanawake, vijana na wazee.

Aidha halmashauri zote nchini zimeagizwa kuunda vikundi maalum vya vijana, walemavu ,wanawake na wazee katika maeneo yao  ili viweze kujiunga na mfumo wa NeST katika maombi ya zabuni mbalimbali za serikali

Agizo hilo limetolewa jana Jujj 14, 2025 Jijini Arusha Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt.Dorothy Gwajima aliyekuwa akimwakilisha Waziri wa Fedha, Dkt,Mwigulu Nchemba wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 9 la Ununuzi wa Umma la Mwaka 2025. 

Katika kongamano hilo lenye kaulimbiu ya ununuzi wa Umma Kigiditali kwa Maendeleo Endelevu, Ukuzaji wa Kampuni na Makundi maalum kwa Ukuzaji wa Kampuni za Wazawa na Makundi Maalum kwa Ukuaji wa Uchumi Jumuishi limeshirikisha zaidi ya washiriki 1500.

Dkt. Gwajima amesema Zabuni hizo zinapaswa kutolewa kwa  makundi maalum ili kuwanyanyua kiuchumi na kwamba hiyo ni dhamira ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwezesha makundi maalum.

Amesema sekta ya ununuzi wa umma inatumia zaidi ya asilimia 70 ya bajeti  ya serikali  katika jitihada za kujenga uchumi wa nchi kwa kuwa mfumo huo umeongeza uwazi ikiwemo kuimarisha utawala bora na kuongeza wigo wa utendaji ikiwemo mapambano dhidi ya rushwa.

"Mifumo ya ununuzi wa umma imeondoa changamoto katika upatikanaji wa zabuni ikiwemo kupunguza matumizi ya karatasi yanayopelekea mazingira kuharibika kutokana na matumizi ya karatasi"amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dennis Simba amesema kupitia mfumo wa Nest mamlaka hiyo imeweza kusajili jumla ya wazabuni 38,163 ambapo kati ya hao wazabuni 36,377 ni wazabuni wa ndani na 1,786 ni wazabuni kutoka nje ya nchi. 

Amesema pia taasisi za ununuzi 61,415 zikiwemo taasisi kuu ngazi za chini  za serikali za mitaa zimesajiliwa na NeST.

"kwa mwaka 2024/25 hadi kufikia Juni 2025 jumla ya taasisi nunuzi 20,954 zilitangaza mipango ya ununuzi  yenye thamani ya zaidi ya sh , trillion 30 ambapo jumla ya zabuni 258,787 zimetangazwa huku zabuni 140,494 zilitolewa zenye thamani ya sh, trilioni 8.6 huku taasisi za ununuzi 1,701 pamoja na shule na vituo vya afya 59,714 zinatumia mfumo wa Nest,"amesema.

Amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/24 utafiti uliofanywa na PPRA umebaini matumizi ya mfumo wa NeST umepunguza metariki  tani 617.85 za utoaji wa kaboni anga uliosaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya kuchapisha karatasi.

" kiasi hicho cha metariki kimeondosha magari 144 yanayotumia mafuta ya diseli barabarani kila mwezi, tangu kuanza kwa mfumo wa NeST umepelekea vikundi 578 kusajiliwa na kuanza kutumia mfumo huu kwa kuomba zabuni zinazotolewa na taasisi za serikali ambapo jumla ya tuzo 501 zenye thamani ya sh, bilioni 16.1 zimewez kutolewa kwa makundi maalum," amesema na kuongeza:

"Tutoe vipaumbele kwa makundi maalum na vikundi vingine ili waweze kuomba zabuni katika taasisi na halmashauri mbalimbali nchini ili wajikwamue katika uchumi jumuishi" amesema.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha,Dk, Natu Mwamba amesema jumla ya vikundi 500 vimesajiliwa na kuzitaka   kuchamkia zabuni mbalimbali zinazotolewa kupitia mfumo wa NeST sanjari na kuziomba taasisi mbalimbali kutekeleza takwa la kutenga asilimia 30 kwaajili ya makundi maalum yaliyopo nchini ili kunufaika na manunuzi na kuepuka utegemezi kwaajili ya kujikwamua katika uchumi jumuishi

Mwisho


 Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dennis Simba, akizungumza.


Post a Comment

Previous Post Next Post