Kaimu mkuu wa mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Kahama Mboni Mhita, akizungumza.
Na Mwandishi Wetu, Kahama
Kwa mwaka wa pili mfululizo Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga imepata hati safi kutoka ofisi ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG).
Akizungumza katika mkutano maalum wa baraza la madiwani uliofanyika June 16, kujadili taarifa ya majibu ya hoja na mpangokazi wa utekelezaji wa mapendekezo ya taarifa ya CAG, kuhusu hesabu za Halmashauri ya Ushetu mwaka wa fedha 2023/2024, kaimu mkuu wa mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Kahama Mboni Mhita ameipongeza Halmashauri kwa kupata hati hiyo.
Mboni ametoa rai kwa madiwani kuendeleza ushirikiano baina yao na wataalamu wa Halmashauri uliofanikisha kupatikana kwa hati hiyo, sambamba na kuendelea kusimamia makusanyo yanayopatikana ili kuendelea kuwahudumia wana-Ushetu kama ilivyo azma ya serikali.
Ameishauri Halmashauri hiyo kuhakikisha inasimamia upatikanaji wa hati miliki ya eneo litakalotumika kujenga makao makuu ya Halmashauri hiyo, ili kuondoa migogoro na wananchi wasio waaminifu wanaovamia maeneo ya serikali na kudai ni ya kwao huku wakitaka kulipwa fidia.
“Serikali imeleta fedha nyingi sana, na pale tunaenda kujenga mradi wa kiutawala ambao Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan amehakikisha kila Halmashauri inapata jingo la kisasa la utawala kwa ajili ya watumishi wa Halmashauri” Amesema Mboni
Na kuongeza “Sasa itakuwa ni kitu cha ajabu mabilioni ya fedha yaende sehemu ambayo hati bado haijakamilika, natambua lipo kwenye taratibu lakini kupitia baraza hili mheshimiwa mwenyekiti tushauri taratibu za upatikanaji wa hati liweze kwenda kwa haraka”
“Hii dunia ya leo anaweza akaibuka tu mtu akasema eneo ni la kwake, kwa sababu tunatambua baadhi ya watu wana nia ovu, japo tunatambua ni la halmashauri miaka na miaka lakini ni vyema tukakamilisha taratibu za kisheria ili kuondoa sintofahamu hizo” Amesisitiza Mboni
Kuhusu ukamilishaji wa miradi amesema hakuna sababu za kutokamilishwa kwa miradi, akatumia baraza hilo kuitaka kila Halmashauri wilayani humo kukamilisha miradi yake kwa wakati badala ya kusubiri mwaka wa fedha unamalizika na fedha zinarudi kwenye mfumo huku wananchi wakihitaji huduma.
“Kama tukipendelewa tukapewa fedha kwa ajili ya mradi Fulani, ikirudi tafsiri yake ni kwamba hamko tayari kutekeleza huo mradi, kwa hiyo nawaomba sana mapenzi aliyonayo Rais wetu kwa wananchi wake tuyaishi, tusimwangushe”
Amewataka wataalamu wa Halmashauri hiyo kuendelea kusimamia miradi ya maendeleo sambamba na kufanyia kazi mapendekezo ya CAG kukamilisha hoja zilizobaki.
KUHUSU UCHUMI WA WANANCHI WA KAHAMA,
Mboni amewataka wakazi wa Kahama kuchangamkia fursa ya uwepo wa mikopo ya asilimia kumi kwenye Halmashauri ikiwemo asilimia 2 kwa ajili ya watu wenye ulemavu, asilimia 4 kwa akina mama na asilimia 4 kwa vijana.
Amewataka watumishi wa Halmashauri wenye dhamana na mikopo hiyo kufuatilia na kuhakikisha urejeshaji wa fedha hizo ili kuendelea kuwakopesha wengine wenye uhitaji na kuwakwamua na umasikini.
“Katika kitu ambacho Mheshimiwa Rais hataki kukiona ni kuona wananchi wananung’unika, wanasikitika au wanapata tabu, sasa ndugu zangu hakuna kikubwa cha kumshukuru mheshimiwa Rais zaidi ya kumuunga mkono kwa kazi kubwa anayoifanya, kumuombea afya njema, Octoba tukatiki, lakini na madiwani tukawahamasishe wananchi wetu wajitokeze wapate hizi fedha” Amesema Mboni
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ushetu Gagi Lala amesema mafanikio yanayopatikana yanatokana na ushirikiano uliopo kati ya madiwani, ofisi ya mbunge na wakuu wa idara ofisi ya mkurugenzi, na kutoakana na mfumo wao sahihi wanaamini watafika mbali zaidi.
“Lakini kwa sababu ya mshikamano, umoja na utulivu tulionao wana-Ushetu kuanzia kwa madiwani, mbunge pamoja na wakuu wa idara ofisi ya mkurugenzi ndio silaha pekee iliyotuvusha leo tukafikia kwenye mwonekano huu” Amesema Gagi
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ushetu, Essery Pima, amesema tayari ofisi yake imeandaa mpango kazi wa utekelezaji wa mapendekezo ya CAG, kwenye hoja zilizosalia, na kila mkuu wa idara amepewa majukumu ya kushughulikia hoja husika ndani ya muda uliopangwa.
"Tumepokea mapendekezo ya CAG tutaendelea kufanyia kazi kama ilivyoelekezwa, Timu tunayo ila na ahidi kuendelea kusimamia na wakuu wa idara ili tuweze kujibu hoja za CAG kwa wakati na kwa mwaka 2024/2025 tunaamini kwamba yako mengi ambayo tayari tumeyafanyia kazi kama CAG alivyotuelekeza", amesema Essery.
Kwa upande wake Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali Mkoa wa Shinyanga CPA Yusuph Mambwe, amesema baadhi ya hoja ambazo zimehakikiwa na kufungwa zimebaki na mapendekezo kadhaa ambayo yako katika hatua za utekelezaji.
Amesema katika mwaka 2024/2025, atafanya ufuatiliaji wa mapendekezo aliyoyatoa na yatakapokamilika mkurugenzi na timu yake watatakiwa kuwasilisha vielelezo.
“Kaguzi zetu zimefanyika kwa mujibu wa matakwa ya ibara ya 143 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na kifungu namba 10 cha sheria ya ukaguzi ya umma, sura namba 418”
“Hivi vyote kwa pamoja vinamtaka mdhibiti na mkaguzi mkuu wa Hesabu za serikali (CAG) kufanya kaguzi za fedha na uzingatiaji wa kanuni na sheria mbalimbali kwenye taasisi za umma angalau mara moja kwa mwaka na hivyo tulifanya hivyo na kutoa mapendekezo kadhaa” Amesema Mambwe
Diwani wa kata ya Kinamapula Sharif Samwel akizungumza wakati wa baraza hilo ameiomba Halmashauri kuendeleza mazuri yaliyopo ili Ushetu iendelee kuwa na hati safi.
MWISHOO
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ushetu Gagi Lala, akizungumza.
Kaimu mkuu wa mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Kahama Mboni Mhita, akizungumza.
Post a Comment