Na Mwandishi wetu, Kagera
Katika tukio lililoshuhudiwa hivi karibuni, wanachama 67 wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutoka kata mbalimbali za wilaya ya Missenyi mkoani Kagera, kuamua kuondoka katika chama hicho na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM) hali hiyo uwenda imeibua maswali na sintofahamu kati ya wananchi na viongozi wachache baada ya kusikia taarifa hiyo kupitia vyombo mbalimbali vya habari.
Tukio la wanachama hao kuondoka Chadema lilifanyika Juni 29, 2025, ambapo wanachama hao walikusanyika katika Ofisi za CCM wilayani Missenyi ili kurejesha kadi zao za CHADEMA na kujiunga na chama cha mapinduzi (CCM) wakimuunga mkono Evance Kamenge, ambaye anagombea kiti cha ubunge katika Jimbo la Missenyi.
Akizungumzia hali hiyo Mkongwe katika siasa, Valerian Rugalabamu, ameeleza kuwa hana shaka na uhamaji huo huku akisisitiza kuwa hali hiyo imekuwa ikijitokeza kwa muda mrefu na kwa vipindi tofauti huku akiongeza kuwa hakuna sababu ya wananchi au viongozi kuwa na mawazo tofauti kuhusu uhamaji huo.
Amesema kuwa yeye ni mpenzi wa demokrasia hivyo na watu wana haki ya kuchagua chama wanachotaka.
Rugalabamu ametoa kauli hiyo kupitia vyombo vya habari Julai mosi,2025 baada ya kuhojiwa juu ya masuala mbali mbali ya kisiasa katika wilaya ya Missenyi ambapo amesema kuwa ametoa ushauri kwa wanachama hao baada ya wao kumfikia na kutaka awashauri juu ya namna ya kurejesha kadi zao kutoka Chadema kwenda CCM.
" Niliwashauri Mimi mwenyewe baada ya wao kuniomba utaratibu watakaoutumia wa kurejesha fomu"alisema Velerian.
Aidha, ameongeza kuwa wengi wa wanachama hao walieleza sababu za kuhama kuifuata CCM kuwa ni kuvutiwa na utendaji wa Rais Samia na Evance Kamenge, ambaye ana maono ya kukiimarisha chama hicho kiuchumi na kijamii baada ya kutia nia ya kugombea nafasi ya ubunge Jimbo la Missenyi Mkoani Kagera.
Katika upande wake, Evance Kamenge ameeleza furaha yake juu ya uhamaji huo na kusema kuwa inapendeza kama wanachama hao wameamua kuhama kwa mapenzi yao wenyewe na kuja kwenye chama chake CCM pia kuvutiwa na maono na sera nzuri huku akimshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema hiyo.
Kamenge amesema kuwa ana dhamira ya kuijenga Missenyi yenye maono mapya na kuwa tayari ameshuhudia watu mbali mbali wa wilaya ya Missenyi wakimwambia kuwa awabariki wamkabidhi kadi za Chadema ili wajiunge na CCM ambapo amekuwa akiwaelekeza kufuata taratibu za kuwasiliana na katibu wa chama katika kata ili wapate maelezo zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo mpaka sasa zaidi ya watu 100 kutoka kata ya Kitobo na Kanyigo wilayani Missenyi wanafuatilia kwa karibu taratibu za kurejesha kadi zao Chadema ili wajiunge na Chama Cha Mapinduzi CCM.
Ikumbukwe kuwa katika tukio la hivi karibuni, wanachama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakiwemo Remigius Daniel, Salum Masoud, Jackline Joseph, Ramadhan Abdalla, Apornary Joseph, Martin Mathias, Ailin John, Mariana Thomas, na Elivia Karoli, wameamua kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM).
Naye Katibu wa CCM wilaya ya Missenyi Bakhari Mwacha, aliweka wazi kuwa amewapokea wanachama hao na kwamba tayari wamerudisha kadi zao ili kujiunga na chama hicho.
Mwacha aliwataka wanachama hao kuwa wavumilivu wakati mchakato wa kutengeneza kadi zao kwa mfumo wa kidijitali ukiendelea.
Hata hivyo amehakikishia kuwa taarifa zao zitafikishwa makao makuu ya CCM na kadi zitawafikia kupitia Katibu wa tawi katika kata zao.
Post a Comment