" MWARABU: UCHAGUZI HUU MSINUNULIWE KWA VITENGE NA HELA, CHAGUENI KIONGOZI BORA

MWARABU: UCHAGUZI HUU MSINUNULIWE KWA VITENGE NA HELA, CHAGUENI KIONGOZI BORA

Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Mwarabu Akim akizungumza kwenye semina katika kanisa la RAGT Kitangili Manispaa ya Shinyanga.

Na Mapuli Kitina Misalaba


Katika harakati za kuhamasisha jamii kuhusu kupinga ukatili na kuchagua viongozi bora kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025, Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Mkoa wa Shinyanga imehudhuria semina maalumu katika Kanisa la RAGT lililopo Kitangili Manispaa ya Shinyanga, ambapo waumini wamepata nafasi ya kufundishwa masuala ya maadili, haki, na ustawi wa familia.

Akizungumza katika semina hiyo, Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Mwarabu Akim ametoa wito kwa wananchi na waumini kutokubali kununuliwa kwa pesa au zawadi katika kipindi cha kampeni kuelekea uchaguzi wa 2025.

“Tunaelekea kwenye uchaguzi wa viongozi wa taifa letu. Tuchague kwa busara. Tusikubali kiongozi anayekuja na rushwa ya hela au vitenge atupumbaze. Huyo akishinda, hatakuwa na uchungu na sisi. Atakuwa anaangalia namna ya kurudisha alichotumia badala ya kutatua changamoto zetu,” amesema Mwarabu.

Mwarabu amesisitiza kuwa upigaji kura siyo tukio la kawaida bali ni uamuzi wa miaka mitano wa maendeleo au kurudi nyuma kwa jamii.

“Huu siyo wakati wa mihemko wala ugomvi. Uchaguzi si vita, ni nafasi ya kuchagua kwa akili. Tusikilize hoja za wagombea, si misuli au maneno matamu ya kununua dhamira zetu,” ameongeza.

Katika mjadala huo wa semina, Mwarabu pia ametoa elimu kuhusu aina mbalimbali za ukatili unaoitesa jamii, ikiwemo ukatili wa kimwili, kingono, kisaikolojia, na kiuchumi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa SMAUJATA Manispaa ya Shinyanga, Meryester Nyalusanda amewataka wazazi na walezi kuwalea watoto katika maadili mema, akisisitiza kwamba matumizi ya maneno mabaya na adhabu zisizo na busara kwa watoto hujenga kizazi kilichovunjika kisaikolojia.

“Watoto ni kioo cha familia. Wakiwa wameharibika ni jamii yote imeharibika. Tuwape maneno ya matumaini na siyo ya kuwadhalilisha. Tuwaadhibu kwa hekima pale wanapokosea ili kuwajenga, si kuwavunja moyo,” amesema.

Nyalusanda pia ametumia nafasi hiyo kukemea tabia ya baadhi ya wanawake walokole kuwadharau waume zao kwa kisingizio cha kuwa "wameokoka".

“Wanawake tumekuwa na changamoto moja, hasa sisi walokole. Tumekuwa na tabia ya kuwa bize na maombi, kiasi kwamba baadhi ya wanawake wakishaingia rohoni, wanasahau kwamba baba (mume) naye anahitaji huduma”.

“Kuna wakati mume wako anakuhitaji apate haki yake ya msingi ya ndoa kwa wakati sahihi, lakini badala ya kumjali, unamuita pepo. Unamtamkia: 'We popo, hujui kama nimefunga?' Wakati maandiko yanasema kabla ya jambo lolote, mshauriane na muelewane”.

“Inamaanisha kwamba kabla hujafunga, unatakiwa kumshirikisha mume wako mapema ili ajue, kuliko kumkurupusha. Haya mambo ndiyo yanasababisha ndoa nyingi kuyumba na kuharibika”.

“Tumeokoka, lakini ndoa zetu zina migogoro. Siri ni nini?, Ni kwa sababu wanawake tunajiweka kama vile tumekuwa watakatifu kuliko waume zetu”.

“Ukumbuke kwamba kabla ya kwenda kanisani, mume wako ni muhimu sana kuliko hata mtumishi wa Mungu au baba yako wa kiroho, kwa hiyo wanawake tubadilike. Tuwe mfano mwema katika jamii.”

Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA Manispaa ya Shinyanga, Kabizi Gombo, ameeleza kuwa watoto wengi wanakumbwa na ukatili wa kunyimwa haki zao za msingi kama elimu, chakula, na malezi bora, akisema ni wajibu wa jamii kuhakikisha mtoto analelewa kwa upendo na si kwa manyanyaso.

Naye Katibu wa SMAUJATA Manispaa ya Shinyanga, Husna Maige, amesema SMAUJATA ipo kwa ajili ya kupaza sauti dhidi ya ukatili wa aina yoyote mahali popote.

“Malengo yetu ni kuhakikisha kila sauti ya mnyonge inasikika. Tunasimama na kila mmoja anayepitia ukatili. Hatutafumbia macho vitendo vinavyohatarisha ustawi wa jamii,” amesema Husna.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Idara ya Wanawake na Makundi Maalum wa SMAUJATA Manispaa ya Shinyanga, Leokadia Daudi, amewataka wanawake kuwa mstari wa mbele katika kutetea amani ya ndoa kwa kuepuka vitendo vya ukatili dhidi ya waume zao, ikiwemo kuwakosesha heshima na haki zao.

“Wanawake tukitaka ndoa zetu zidumu, lazima turejee kwenye heshima, utiifu na mawasiliano yenye hekima. Kuolewa si kufungwa, bali ni kushirikiana kwa upendo na maelewano.”

Kwa upande wake, Askofu Jacob Sallu wa Kanisa hilo la RAGT amewapongeza viongozi wa SMAUJATA kwa kufikisha ujumbe muhimu wa kupinga ukatili, huku akiwahimiza waumini kuwa mabalozi wa amani na maadili mema katika familia zao.

Naye Askofu Enock Ndezi wa Kanisa la RAGT kutoka Dar es Salaam, amepongeza juhudi zinazofanywa na viongozi wa SMAUJATA kwa kuwafikia waumini kwa elimu yenye kujenga na kuhamasisha mabadiliko chanya katika jamii.

Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Mwarabu Akim akizungumza kwenye semina katika kanisa la RAGT Kitangili Manispaa ya Shinyanga.


Askofu Jacob Sallu wa Kanisa hilo la RAGT, akitoa mahubiri yake.

Mwenyekiti wa SMAUJATA Manispaa ya Shinyanga, Meryester Nyalusanda, akitoa elimu ya masuala ya ukatili katika kanisa la RAGT lililopo Kitangili mjini Shinyanga.














 


Post a Comment

Previous Post Next Post