Na Mapuli Kitina Misalaba
Tamasha la Utamaduni wa Msukuma (Shinyanga
Sukuma Festival Season 4 ) linalolenga kuenzi na kuendeleza utamaduni wa
kabila la Kisukuma linaendelea kufana katika viwanja vya shule ya msingi
Nhelegani, Kata ya Kizumbi, Manispaa ya Shinyanga.
Tamasha hilo lililozinduliwa rasmi
Julai 18, 2025, linatarajiwa kufikia kilele chake Julai 20, ambapo maelfu ya
wakazi wa Mkoa wa Shinyanga na mikoa jirani wameshuhudia michezo ya asili,
ngoma za utamaduni, mavazi ya jadi, pamoja na bidhaa mbalimbali zikiuzwa na
kuonyeshwa katika mabanda ya maonesho.
Akizungumza
wakati wa kuendelea kwa tamasha hilo, muandaaji wake ambaye ni Mkurugenzi wa THE BSL INVESTMENT COMPANY LIMITED
AND THE TRUE LIVE FOUNDATION Bwana Peter Frank (MR. BLACK) amesema tamasha hilo lina malengo
manne makuu ambayo ni:
1.
Kuendeleza utamaduni wa Msukuma
ulioimara, thabiti na makini.
2.
Kutoa fursa kwa wajasiriamali,
wafanyabiashara na wadau mbalimbali kutoka Shinyanga na mikoa ya jirani kama
Mwanza, Tabora, Geita, Singida na Dodoma kuonyesha huduma na bidhaa zao.
3.
Kuendeleza mshikamano wa kifamilia
kwa kukumbuka mila, upendo na urithi kutoka kwa mababu waliotangulia, wakiwemo
watawala wa jadi kama mtemi Kudililwa wa Kizumbi.
4.
Kuelimisha na kuhamasisha jamii
kushiriki kikamilifu uchaguzi mkuu wa 2025 kwa amani na utulivu chini ya
kaulimbiu ya mwaka huu: “Utamaduni wetu, urithi wetu – Shiriki uchaguzi mkuu
2025 kwa amani na utulivu.”
“Tamasha hili limekuwa dira ya maendeleo katika jamii ya
Shinyanga. Kwanza limeleta fursa za kiuchumi kupitia mabanda ya maonyesho, pili
limefungua milango kwa vijana na vikundi vya asili kuonyesha vipaji na
kuhifadhi tamaduni zao, na tatu linaongeza pato la ndani la Manispaa ya
Shinyanga kutokana na wageni wengi wanaokuja kushiriki,” amesema Mr. Black.
Mr. Black ameongeza kuwa tamasha
hilo limepokelewa vyema na wadau wa utamaduni nchini ambapo limeorodheshwa na
Wizara ya Utamaduni kuwa miongoni mwa matamasha matano bora ya utamaduni
Tanzania. Pia limetambulika kimataifa kutokana na uwepo wa wageni kutoka
mataifa mbalimbali Afrika na nje ya Afrika wanaofuatilia shughuli za tamaduni
zinazofanyika kwenye tamasha hilo.
“Tunaomba tamasha hili litambulike rasmi na serikali ya Mkoa
wa Shinyanga, kwa heshima ya utawala wa jadi wa mtemi Kidola wa Kizumbi.
Litambuliwe kama tamasha la kudumu, lipate vibali na sapoti rasmi ili liweze
kukua zaidi na kufikia hadhi ya kitaifa na kimataifa,” amesema Mr. Black.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa
Wilaya ya Shinyanga, Said Kitinga, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya kama
mgeni rasmi, amempongeza Mr. Black kwa kuwa kijana mwenye dira, ambaye
ameonesha mfano kwa kutumia nguvu zake kuhifadhi na kuendeleza utamaduni wa
Mwafrika, hususan wa Wasukuma.
“Kwanza kabisa, ninampongeza Mr. Black kwa moyo wake wa
kizalendo na uzalishaji wa fikra chanya kwa jamii. Ametusaidia kutambua utajiri
mkubwa uliopo katika utamaduni wetu wa Kisukuma. Kwa niaba ya Serikali,
tunathibitisha kuwa tamasha hili linatambulika rasmi na litaendelea kutambulika
siku zote,” amesema Kitinga.
Washiriki mbalimbali wa tamasha hilo
wametoa pongezi kwa Mr. Black na waandaaji wengine, wakisisitiza umuhimu wa
kulifanya tamasha hilo kuwa la kudumu kila mwaka ili kuendeleza urithi wa
mababu na kuhamasisha vijana kuenzi mila na desturi zao.
Tamasha la Utamaduni wa Msukuma
mkoani Shinyanga lilianzishwa rasmi mwaka 2022 likiwa na kaulimbiu ya kudumu “Lejigukulu
lya Nzengo” likimaanisha sherehe au sikukuu ya jamii ya watu wa jadi, na
limeendelea kuwa jukwaa muhimu la kutangaza utalii wa kitamaduni, kuunganisha
jamii na kuongeza thamani ya urithi wa Kisukuma nchini Tanzania.
Muandaaji
wa tamasha hilo ambaye ni Mkurugenzi wa
THE BSL INVESTMENT COMPANY LIMITED AND THE TRUE LIVE FOUNDATION Bwana Peter
Frank (MR. BLACK) akizungumza.
Katibu Tawala wa Wilaya ya
Shinyanga, Said Kitinga, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga.
Post a Comment