
Na Mapuli Kitina Misalaba
Tamasha la Shinyanga Sukuma Festival Season 4
limehitimishwa Julai 20, 2025 kwa shamrashamra za michezo ya asili, burudani ya
ngoma za jadi na ushiriki mkubwa wa wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa
wa Shinyanga na mikoa jirani.
Akifunga tamasha hilo kwa heshima na mila za jadi, Mgeni
rasmi ambaye ni Mwenyekiti wa Machifu Mkoa wa Shinyanga, Chifu Kidola Njange,
ametangaza rasmi kumsimika Mr. Black kuwa msaidizi wake wa heshima, ndani ya
himaya ya utemi wa Kizumbi, ikiwa ni kutambua mchango wake mkubwa wa kulinda,
kukuza na kuendeleza utamaduni wa Kisukuma.
Katika hotuba yake, Chifu Kidola amewaasa wananchi
kuendelea kuenzi mila na desturi njema zilizoasisiwa na watemi waliotangulia,
akisema utamaduni ni nguzo ya taifa na sehemu ya amani.
“Tuendelee kuitunza amani ya nchi yetu
kupitia mila zetu. Tuishi kwa mshikamano, upendo na heshima kama tulivyolelewa
na mababu zetu. Mwaka huu tunakwenda kwenye uchaguzi mkuu, nawaomba mshiriki
kwa amani, mchangie viongozi bora watakaolinda utu, maendeleo na mila zetu,”
amesema Chifu Kidola.
Kwa upande wake, Mr. Black ambaye ndiye muasisi na
muandaaji mkuu wa tamasha hilo, ameushukuru uongozi wa jadi kwa heshima hiyo
kubwa, na kueleza kuwa tamasha hilo ni endelevu na litazidi kuwa kubwa kila
mwaka.
Ameeleza kuwa kuanzia mwakani 2026, tamasha hilo
litabadilika jina na kuitwa rasmi "SHINYANGA KIZUMBI SUKUMA
FESTIVAL", ili kuipa heshima ya kudumu historia ya utemi wa Kizumbi na
mizizi ya utamaduni wa Wasukuma.
“Ninawashukuru sana wananchi,
wafanyabiashara, viongozi wa serikali, machifu, vikundi vya utamaduni, taasisi
na kila mmoja aliyeshiriki kwa namna yoyote. Tumeandika historia ya utamaduni
wetu – historia ambayo haifutiki,” amesema Mr. Black.
Katika uwanja wa shule ya msingi Nhelegani, ambapo
tamasha hilo limefanyika kwa siku tatu mfululizo, maelfu ya wananchi walijitokeza
kushuhudia ngoma za jadi, maigizo ya asili, mavazi ya kitamaduni, pamoja na
mabanda ya maonyesho ya bidhaa na huduma kutoka kwa wafanyabiashara wa ndani.
Washiriki wengi wameomba tamasha hilo liwe la kudumu
na lijumuishwe rasmi katika kalenda ya matukio ya utamaduni ya taifa, wakisema
linaongeza mshikamano wa kijamii, kukuza uchumi na kutangaza utambulisho wa
Mtanzania kwa mataifa ya nje.
Tamasha la Sukuma Festival lilianzishwa mwaka
2022 chini ya kaulimbiu ya “Lejigukulu vya Nzengo” likiwa na dhamira ya
kulinda urithi wa Kisukuma, na mwaka huu limeorodheshwa rasmi kuwa miongoni mwa
matamasha matano bora ya kiutamaduni nchini Tanzania kwa mujibu wa Wizara ya
Utamaduni.
Post a Comment