Na Lydia Lugakila, Misalaba Media
Bukoba
Devota Daniel Mburarugaba na Samila Khalfan Amour wamejipatia ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Wabunge Viti Maalum Mkoa wa Kagera, wakijishindia nafasi hizo baada ya uchaguzi wa kihistoria uliohudhuriwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) mkoani Kagera.
Katika matokeo yaliyotangazwa, Devota Mburarugaba aliongoza kwa kupata kura 1,308, wakati Samila Khalfan Amour akifuata kwa kura 1,250.
Ushindi wao umetangazwa rasmi, na sasa watawakilisha Mkoa wa Kagera katika Bunge.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, Devota Mburarugaba aliwashukuru wajumbe kwa imani yao, akiahidi kufanya kazi kwa karibu nao katika kuimarisha chama na kuhakikisha wanakusanya kura nyingi kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa upande wake, Samila Khalfan Amour alieleza kuwa ushindi huu ni alama ya umoja wa wanawake wa Kagera, akiahidi kuifanya kazi kwa juhudi kubwa ili kuimarisha chama na kuleta maendeleo katika mkoa huo.
Kulingana na Katibu wa UWT Mkoa wa Kagera, Rehema Zuberi, jumla ya wajumbe 1,556 walihudhuria na kupiga kura katika uchaguzi huu, ambao ulisimamiwa na wasimamizi wawili na kuridhiwa na Kamati Kuu ya UWT Taifa.
Ushindi huu wa wanawake wawili kutoka Kagera unatoa taswira nzuri ya ushirikiano na mshikamano miongoni mwa wanawake katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii na kisiasa.
Post a Comment