Na Lucas Raphael, Tabora MWENGE wa Uhuru umezindua miradi 7 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya sh bil 19.1 katika Halmashauri ya Manispaa Tabora na kumpongeza Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji kwa usimamizi mzuri wa miradi hiyo.Akizungumza kwa nyakati tofauti akiwa katika eneo la miradi hiyo jana Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka huu Ismail Al Usi alionesha kuridhishwa na kazi nzuri iliyofanyika ikiwemo ubora wa miradi hiyo.Amebainisha kuwa miradi hiyo iliyopo katika sekta ya elimu, afya, huduma za utawala, uwezeshaji wananchi kiuchumi na miundombinu ya barabara imeakisi dhamira ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuboresha maisha ya wananchi.Amesisitiza kuwa serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia imeleta mabilioni ya fedha hizo ili kuhakikisha huduma za wananchi zinaboreshwa katika sekta zote, kulinda mazingira na kuinua uchumi wa wananchi.Kiongozi huyo ametoa kongole kwa Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya hiyo chini ya Uenyekiti wa Mkuu wa Wilaya Upendo Wella na Mkurugenzi Mtendaji Dkt John Pima kwa kusimamia kwa dhati utekelezaji miradi hiyo.Ametoa wito kwa wakazi wa manispaa hiyo kutunza vizuri miradi hiyo na kwa vikundi vilivyowezeshwa mikopo itokanayo na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri kuitumia kwa kazi iliyokusudiwa ili waweze kujikwamua kiuchumi.Amedokeza kuwa ubora wa miradi hiyo unaonesha jinsi Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa manispaa hiyo walivyosimamia na kutekeleza maelekezo ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa weledi na ufanisi mkubwa. Ukiwa katika halmashauri ya manispaa hiyo jana Mwenge wa Uhuru umetembelea, kukagua na kutoa cheti kwenye mradi wa sh milioni 345 wa ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na Maabara ya Kituo ya afya Itetemia.Miradi mingine ni wa kikundi cha vijana wa kurekodi na kurusha matukio (kazi digital) uliowezeshwa na halmashauri hiyo mkopo wa sh mil 50 na ujenzi wa km 2.4 za barabara ya lami unaogharimu sh bil 3 eneo la maili tano Ipuli.Mradi wa uhifadhi mazingira na utumiaji nishati safi na salama ya kupikia unaotekelezwa na Gereza Kuu la Uyui uliogharimu sh mil 20.7, ujenzi ofisi ya Kata Isevya (sh mil 81), uhifadhi chanzo cha maji Bwawa la Igombe (sh bil 1.8) na uboreshaji miundombinu ya shule ya sekondari Kazima (sh mil 160).Mwisho 

Post a Comment