Na Lucas Raphael, Misalaba Media -Tabora
Katika hali ya kusikitisha watu wanne wa Kijiji cha Bulumbela Kata ya Ziba Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora, akiwemo Katibu wa CCM na Mwenyekiti wa Kitongoji wamejeruhiwa vibaya na Mnyama aina ya Fisi wakiwa Kijijini kwao.
Mtendaji wa Kijiji cha Bulumbela Idd Makalo alisema tukio hilo limetokea Julai 14, 2025 majira ya saa mbili asubuhi wakati wananchi hao wakitekeleza majukumu yao.
Alisema Fisi huyo alitokea kwenye makazi hayo ya wananchi na kuanza kuwajeruhi wananchi hao ambao aliwataja majina yao ni Maganga Nkwande ambaye ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mbuyuni, Busongo Malekela ambaye ni Katibu wa CCM Tawi la Bulumbela, Juma Masanilo na Tatu Kabeya.
Mtendaji huyo wa Kijiji alisema baada ya wananchi kuona wenzao wakishambuliwa na kujeruhiwa walipiga mayowe ambapo wananchi walianza kumshambulia kwa silaha za jadi mikuki, mapanga, shoka hadi kufanikiwa kumuua.
Alisema baada ya kuuwawa Fisi huyo wananchi waliamua kugawana viungo vyake na kuondoka navyo.
Hata hivyo Mtendaji huyo alisema wananchi wote waliojeruhiwa waliwachukua na kuwakimbiza Kituo cha Afya Ziba ambapo walipatiwa matibabu.
Kufuatia tukio hilo Mtendaji aliwasihi wananchi wake kuwa makini na wanyama wakali na hatarishi kama hao Fisi, lakini pia kuepuka kutembelea maeneo hatarishi kama vichakani na mapangoni.
Nao baadhi ya wananchi Mrisho Juma na Fadhili Isaya walisema Fisi huyo walipambana naye kwa zaidi ya dakika 45 ambapo alikuwa akirukia kila mtu aliyemsogelea, hata hivyo mwananchi mmoja alifanikiwa kumkata na shoka kichwani hadi kuanguka na kufa pale pale.
“Kwa kweli huyu Fisi siyo wa kawaida kwani wakati tukipambana naye alikuwa akipiga kelele kama binadamu na ndiyo maana tumeamua kugawana viungo vyake vyote”.
Naye Kaimu Mkuu wa Idara ya Maliasili hifadhi ya mazingira wilaya ya Igunga Emanuel Mnanka alithibitisha kuuwawa kwa Fisi huyo, “Ni kweli wananchi walimuua Fisi huyo kwani tulipigiwa simu na Mtendaji wakati tukijiandaa kwenda katika Kijiji hicho tulijulishwa kuwa tayari Fisi huyo wamemuua”.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Igunga Dk. Lucia Kafumu alikiri kupokea majeruhi wanne katika kituo cha Afya Ziba na kusema kuwa waliojeruhiwa wote walipatiwa matibabu mazuri na hali zao zinaendelea vizuri.
Hata hivyo alibainisha kuwa amewataka wagonjwa wote waliojeruhiwa kwenda Hospitali ya Wilaya kwa ajili ya kupatiwa kinga ya chanjo za wanyama.
MWISHO.
Post a Comment