" MADAKTARI BINGWA 36 WA MAMA SAMIA WAWEKA KAMBI YA SIKU TANO MKOANI SHINYANGA, WANANCHI WAKARIBISHWA KUPATA HUDUMA

MADAKTARI BINGWA 36 WA MAMA SAMIA WAWEKA KAMBI YA SIKU TANO MKOANI SHINYANGA, WANANCHI WAKARIBISHWA KUPATA HUDUMA


Na Mapuli Kitina Misalaba

Madaktari bingwa wanaoshiriki katika Kampeni ya Huduma za Kibingwa ya Mama Samia leo wameanza rasmi kambi ya kutoa huduma za kibingwa mkoani Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kambi hiyo, Afisa Programu kutoka Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Dkt. Michael Mbele, amesema kuwa huu ni mwendelezo wa awamu ya nne ya kampeni hiyo inayotekelezwa chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Tuko Shinyanga kwa awamu ya nne ya kampeni ya huduma za kibingwa za Mama Samia. Tunatarajia kufika kwenye halmashauri zote na kutoa huduma kwa wahitaji wote wa huduma za kibobevu. Lengo ni kuwapunguzia wananchi gharama za kufuata huduma hizo katika Hospitali ya Bugando na kuzipata karibu na makazi yao,” amesema Dkt. Mbele.

Amefafanua kuwa huduma zitakazotolewa ni pamoja na huduma za uzazi, huduma kwa watoto na watoto wachanga, magonjwa ya ndani, pamoja na upasuaji wa kibingwa, na kuongeza kuwa wanatarajia kuwahudumia zaidi ya wagonjwa elfu 30 katika awamu hii pekee, huku kwa awamu zilizopita zaidi ya watu laki mbili na arobaini (240,000) wakiwa wameshapata huduma hizo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amepongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuboresha sekta ya afya na kuwaletea wananchi huduma za kibingwa.

“Tunaishukuru sana serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutusogezea huduma hizi muhimu. Zaidi ya wananchi laki mbili na arobaini wamepata huduma kupitia kambi za madaktari bingwa wa Mama Samia, na zaidi ya wataalam elfu 15 wa afya wamejengewa uwezo kutokana na programu hii,” amesema Mhita.

RC Mhita amewahimiza wananchi wa mkoa wa Shinyanga kujitokeza kwa wingi kupata huduma hasa wale wenye magonjwa sugu kama presha, kisukari, figo, na magonjwa ya moyo, akibainisha kuwa huduma hizo zitapatikana kwa siku tano kuanzia leo katika wilaya zote za Kishapu, Shinyanga na Kahama, zikihusisha halmashauri zote sita za Mkoa wa Shinyanga.

Naye, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Yudas Ndungile, amesema ujio wa madaktari bingwa hao 36 ni neema kubwa kwa wananchi wa mkoa huo.

“Tunayo furaha kubwa leo kuwapokea madaktari bingwa 36 hapa mkoani Shinyanga. Manufaa makubwa ni wananchi kupata huduma za kibingwa na za kibobezi bila kulazimika kusafiri mbali kwenda Bugando. Wataalam hawa pia watawajengea uwezo madaktari waliopo katika hospitali zetu za halmashauri na manispaa ili waweze kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi,” amesema Dkt. Ndungile.


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, akizungumza kwenye hafla ya kuwapokea madakatari bingwa 36.


Post a Comment

Previous Post Next Post