
Mkurugenzi wa The BSL Investments na mmiliki wa BSL Schools Tanzania na Rwanda, Ndugu Peter A. Frank Lugumi (maarufu kama Mr. Black), leo Oktoba 8, 2025, anahudhuria mwaliko maalum katika Ikulu ya Uganda.
Tukio hilo limewaleta pamoja wabunge wote wa Uganda, wawekezaji, viongozi mashuhuri, pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo, katika hafla ijulikanayo kama National Prayer Breakfast — tukio la kila mwaka linaloandaliwa na Bunge la Uganda kwa lengo la kukuza umoja, maombi na mshikamano wa kitaifa.
Mr. Black amekuwa nchini Uganda tangu Oktoba 5, 2025, ambapo ameiwakilisha Tanzania katika mkutano mkubwa wa vijana kutoka nchi nane za Afrika ujulikanao kama Africa Youth Leadership Forum.
Mkutano huo unaolenga kukuza na kuandaa viongozi bora wa kizazi kijacho barani Afrika, umehusisha nchi za Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), na Sudan Kusini, na umefanyika katika Botanical Imperial Beach Hotel, Entebbe kuanzia Oktoba 5 hadi 7, 2025.
Katika mkutano huo, Mr. Black aliwakilisha vyema Tanzania kupitia wasilisho lake kuhusu uongozi bora na uimarishaji wa amani barani Afrika, akitumia pia nafasi hiyo kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia miradi ya maendeleo, vivutio vya utalii, fursa za uwekezaji, na kuonesha utamaduni wa kabila la Wasukuma.
Aidha, Mr. Black anatarajiwa kushiriki katika tamasha la utamaduni wa Uganda – Vumbula Festival, litakaloweka msingi wa mahusiano ya kiutamaduni kati ya mataifa haya mawili, hasa kupitia Shinyanga Sukuma Festival ya Tanzania, inayolenga kuhifadhi na kukuza urithi wa kitamaduni wa Wasukuma.
Baada ya shughuli zake nchini Uganda, Mr. Black ataendelea na ziara zake binafsi katika nchi za Rwanda, Zambia na Malawi, zenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, uwekezaji na kubadilishana uzoefu wa kielimu na kijamii.
Kupitia ushiriki wake katika matukio haya muhimu, Mr. Black ameendelea kuwa miongoni mwa vijana vinara wa kuhamasisha amani, umoja na maendeleo barani Afrika, huku akitoa wito kwa vijana wa Tanzania kujitokeza, kushiriki kikamilifu katika mijadala ya maendeleo, na kuendeleza urithi wa uongozi bora unaolenga kuijenga Afrika yenye umoja na ustawi.

Post a Comment