" MZEE BUTIKU AWAPIGA STOP VIJANA WANAOCHEMSHA VURUGU MTANDAONI!

MZEE BUTIKU AWAPIGA STOP VIJANA WANAOCHEMSHA VURUGU MTANDAONI!

Na Mwandishi wetu

Wakati mitandao ya kijamii ikizidi kutumika kusambaza ajenda za uchochezi na malalamiko yanayoelekezwa kwenye maandamano, sauti ya busara ya Mzee Joseph Butiku, Katibu wa zamani wa Baba wa Taifa na Mwenyekiti wa Mwalimu Nyerere Foundation, imevuma tena.

Akizungumza kwa uzito mkubwa wa historia na hekima ya ujenzi wa taifa, Mzee Butiku ametoa onyo kali kwa kizazi kipya: Vurugu haijawahi kumletea mtu faraja—utamaduni wa Tanzania ni kwenda salama na kurejea salama.

Mzee Butiku ameweka wazi kuwa ni muhimu sana kwa Watanzania wote kudumisha maadili, upendo, na misingi ya amani iliyojengwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Hii ni sauti ya tahadhari kwa wote wanaochezea msingi wa utulivu wa taifa kwa maneno ya uchochezi, kauli za kugawa taifa, na propaganda za mitandaoni zinazolenga kuvuruga umoja wa nchi.

Biashara ya Taharuki, Si Maslahi ya Taifa

Kiongozi huyo wa hekima amefichua kuwa ajenda za uchochezi na upotoshaji mtandaoni hazina maslahi kwa taifa, bali ni biashara za taharuki zinazowanufaisha wachache wanaotumika na vibaraka wa nje. 

Kwa muda, kimya cha wazee wa kizazi cha Nyerere kilianza kutumiwa vibaya, huku wanaharakati wa uongo wakijaribu kuhusisha majina ya heshima kama Butiku kwenye ajenda zao za kugawa wananchi. Kauli yake sasa imefuta mashaka yote: Wazee wenye hekima wamesema hapana kwa vurugu, na ndiyo kwa amani.

Mzee Butiku amesisitiza kwa dhati kwamba amani ya Tanzania haikupatikana kwa bahati mbaya; ilijengwa kwa gharama kubwa, kwa damu na jasho la Watanzania waliolinda mipaka ya nchi dhidi ya maadui wa ndani na nje. Ametoa mfano wenye nguvu: wanaharakati hawa wanataka "kusafisha njia" kwa maneno ya chuki, sawa na mjenzi anavyosafisha eneo, ili kujenga mgawanyiko na taharuki.

Utulivu Ndio Nguzo Kuu: Vurugu Haijengi

Akisisitiza kuwa hakuna taifa lolote duniani lililopata maendeleo kupitia vurugu, amewataka Watanzania waendelee kulinda amani, umoja, na mshikamano bila kujali dini, kabila, wala itikadi.

Akichangia mjadala huu, mchambuzi Joe Lugendo amekumbusha jinsi Mwalimu Nyerere alivyotumia kanuni (Codes) za tahadhari kama vile aliyekula nyama ya mtu ataendelea kula na mizengwe. Lugendo anasema anashuhudia jinsi "mizengwe na ulaji wa nyama ya mtu" (yaani mikakati mibaya) imeunganishwa kwa sasa, lakini anaamini hazitafanikiwa kwa sababu Watanzania ni wengi wanaotaka utulivu (Stability) wa Taifa lao.

Lugendo anasisitiza kuwa Watanzania wanajivunia utulivu na amani yao, na hawatavurugwa na kikundi kinachounganisha codes. Anawatakia Watanzania wote Uchaguzi wa amani na utulivu, lakini akaonya kwamba baada ya uchaguzi, masijala ya mitandao itaturejesha kwenye tafakuri mpya kuhusu kanuni ya tatu ya Mwalimu: Code ya Nyufa (migawanyiko).

Huu ni wito wa Kizazi Kipya: Sauti ya Butiku inawakumbusha waigizaji wa taharuki mtandaoni kuwa Tanzania haitavunjwa. Amani haitauzwa. Watanzania wanajua ukweli, wanathamini utulivu, na watasema kwa sauti moja: "Hapana kwa uchochezi, ndiyo kwa amani!"


Post a Comment

Previous Post Next Post