Na RS SHINYANGA
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amefanya kikao kazi na watumishi wa Manispaa ya Shinyanga akiwa katika ziara ya kujitambulisha rasmi, ambapo amesisitiza udhibiti wa mianya ya upotevu wa mapato, uwajibikaji, uadilifu na utatuzi wa changamoto za wananchi.
Akiwa anaongea mbele ya viongozi na watumishi wa halmashauri hiyo, RC Mhita aliwataka wakuu wa idara na vitengo kuhakikisha wanasikiliza na kushughulikia kero za wananchi kwa wakati.
“Si jambo la busara kuona wananchi wanalalamika kuhusu huduma wakati ninyi mpo kazini. Wananchi wanahitaji huduma bora, na ninyi ndio mnapaswa kuwa suluhisho,” alisema kwa msisitizo.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa alitoa maagizo kwa Mkurugenzi wa Manispaa hiyo kuhakikisha mianya ya upotevu wa mapato inazibwa, huku pia akielekeza jitihada za kuongeza vyanzo vipya vya mapato kwa kutumia rasilimali zilizopo ndani ya manispaa hiyo.
“Kila senti inayokusanywa itumike ipasavyo. Tengeni maeneo kwa ajili ya wawekezaji ili kukuza uchumi wa manispaa na kuongeza ajira kwa wananchi wetu,” aliongeza.
Vilevile, Mh. Mhita alisisitiza kwamba miradi yote ya kimkakati ambayo haijakamilika inapaswa kupewa kipaumbele katika utekelezaji na usimamizi wake, ili iweze kuleta matokeo chanya kwa jamii.
Katika hatua nyingine, RC huyo aliitaka Halmashauri kuendelea kutoa hamasa kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika kushiriki uchaguzi mkuu ujao, akisema hiyo ni sehemu muhimu ya kukuza demokrasia na kuwapa wananchi nafasi ya kuchagua viongozi wanaowataka.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Mwalimu Alexcius Kagunze amempongeza RC Mhita kwa kuteuliwa na akaahidi kutekeleza maagizo yote kwa weledi, ikiwemo kusimamia mapato, uwekezaji, miradi ya maendeleo na maandalizi ya uchaguzi.
Baada ya kuzungumza na watumishi RC Mhita alifanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya Maendeleo katika manispaa hiyo ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi katika manispaa hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita
Post a Comment