Kiongozi mstaafu wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema kuwa chama hicho kimejiandaa kukabiliana na kile ilichokitanabaisha kama hujuma dhidi ya mawakala wao wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, ikiwemo kuzuia mawakala kuingia vituoni na kunyimwa nakala za matokeo.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika Jimbo la Tunduru Kusini wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, Zitto amedai kuwa wapo baadhi ya wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ambao hufanya kazi kwa niaba ya chama fulani kwa kuzuia mawakala wa vyama vingine kushiriki kikamilifu zoezi la uchaguzi.
Kwa mujibu wa Zitto, hali hiyo imewahi kujitokeza kwenye chaguzi zilizopita, lakini mwaka huu chama hicho kimejiimarisha kuhakikisha kila hatua ya uchaguzi inasimamiwa ipasavyo.
Amesema pia kuwa moja ya udanganyifu unaofanyika ni pamoja na mawakala kunyimwa fomu ya matokeo mara baada ya kura kuhesabiwa. Kwa mujibu wa sheria, nakala ya matokeo inapaswa kubandikwa nje ya kituo na kutolewa kwa kila wakala.
Zitto amesisitiza kuwa Operesheni Majimaji inaendelea kuhakikisha Watanzania wanapata uchaguzi wa haki kwa kusimamia kura zao wenyewe, na kwamba ACT Wazalendo haitakubali tena hujuma za uchaguzi zisizokemewa.
Post a Comment