Ukusanyaji wa mapato umeendelea kuwa ajenda ya kudumu katika vikao vya Timu
ya Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita, ikiwa ni moja ya nguzo muhimu
ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Katika mwaka wa fedha 2024/2025, Halmashauri hiyo imevunja rekodi kwa kuvuka
lengo la ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 125.19. Jumla ya shilingi bilioni
10.4 zimekusanywa, ikiwa ni ongezeko la shilingi bilioni 2.1 kutoka kwenye
bajeti iliyokasimiwa ya shilingi bilioni 8.3.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Ndg. Karia Rajab
Magaro, amewasihi watendaji wote wa Halmashauri kuendelea kuwa waadilifu na
wabunifu katika usimamizi wa mapato, huku akisisitiza kudhibiti mianya ya
upotevu wa fedha ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji.
Kupitia usimamizi bora wa mapato ya ndani, miradi mbalimbali ya maendeleo
imetekelezwa kwa mafanikio makubwa. Kwa mwaka wa fedha 2024/2025, kiasi cha
shilingi bilioni 3.1 kimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi
inayojumuisha ujenzi wa shule, zahanati, vituo vya afya, nyumba za watumishi na
ofisi za kata.
Aidha, kupitia mapato ya ndani na fedha za marejesho, Halmashauri
imefanikiwa kutoa mikopo ya asilimia 10 kwa makundi maalum ya wanawake, vijana
na watu wenye ulemavu. Jumla ya shilingi bilioni 1.8 zimelipwa kwa wananchi waliokidhi
vigezo vya kupokea mikopo hiyo.
Katika kuimarisha zaidi huduma kwa wananchi, Halmashauri imeendelea na
mkakati wa kutwaa maeneo ya uwekezaji, ikiwa ni hatua ya kuongeza vyanzo vya
mapato na kuendeleza miundombinu ya kijamii na kiuchumi.
Mnamo Julai 24, 2025, Timu ya Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita
ikiongozwa na Kaimu Mkurugenzi, CPA Eveline Ntahamba, ilifanya ziara katika
Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro kwa lengo la kukagua maeneo ya uwekezaji. Ziara
hiyo ilihusisha eneo lenye ukubwa wa hekari 14 linalotarajiwa kutwaliwa kwa
ajili ya ujenzi wa stendi ya mabasi (Katoro Bus Stand) pamoja na soko la
Kariakoo Katoro.
Kwa hatua hizo, Halmashauri ya Wilaya ya Geita inaendelea kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mchango mkubwa wa fedha katika kufanikisha shughuli mbalimbali za maendeleo.
Post a Comment