Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndugu Ismail Ali Ussi, ametoa wito kwa vijana wa Wilaya ya Msalala na Tanzania kwa ujumla kuepuka vitendo vya uhalifu na badala yake kutumia fursa halali kama shughuli za usafirishaji kwa njia ya bodaboda kujipatia kipato kwa njia za uadilifu na nidhamu.Ametoa kauli hiyo katika hafla fupi iliyofanyika katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, wakati wa uzinduzi na makabidhiano ya pikipiki tano zenye thamani ya milioni 13.5 kwa kikundi cha vijana cha *Hatushindwi*, kilichonufaika na mkopo wa asilimia 10 kutoka halmashauri hiyo.Pikipiki hizo zimepatikana kupitia mkopo wa asilimia 10 ya mapato ya ndani, mkopo ambao uliondolewa na kurejeshwa tena na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya awali kusitishwa kutokana na changamoto ya urejeshaji kwa wakopaji.Ussi amesema sekta ya bodaboda imeendelea kuwa mkombozi mkubwa kwa vijana, lakini akasisitiza kuwa ni lazima ajira hiyo ifanywe kwa uaminifu, uwajibikaji na kuepuka kutumia pikipiki hizo kama kichaka cha uhalifu au matumizi ya dawa za kulevya.“Mnatakiwa kuwa waaminifu, mjiwekee malengo. Kazi kama bodaboda ni ajira halali, ichukulieni kwa uzito na siyo uchochoro wa kutenda uhalifu. Amani ya nchi ni jukumu letu sote,” alisema Ussi.Kwa upande wake, Frank Charles, Katibu wa Kikundi cha *Hatushindwi*, ameipongeza Serikali kupitia Rais Dkt. Samia kwa kurejesha mikopo hiyo muhimu kwa vijana na kusema kuwa hatua hiyo imekuwa mwanga mpya kwa vijana wengi waliokosa ajira rasmi.Aidha, wananchi wa Msalala wamehimizwa kuwaunga mkono vijana hao kwa kuwatumia katika huduma za usafiri ili kuhakikisha miradi hiyo inaleta tija kwa jamii na kuwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi miongoni mwa vijana.

Post a Comment