Msalala. Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndugu Ismail Ali Ussi, leo amezindua rasmi Klabu ya Wapinga Rushwa katika Shule ya Sekondari Bumva iliyopo Kata ya Segese, Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, mkoani Shinyanga.Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika kwenye viwanja vya shule hiyo Ussi aliipongeza shule hiyo kwa hatua ya kuanzisha klabu hiyo, akisema ni jitihada muhimu katika kulea kizazi cha vijana waadilifu, wazalendo na wenye uelewa wa mapema kuhusu madhara ya rushwa kwa taifa."Vijana wa klabu hii mmepewa nafasi ya kipekee kuelimika mapema kuhusu athari za rushwa. Mnatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kutoa taarifa pale mnapoona au kusikia dalili za vitendo vya rushwa. Huu ni mchango wenu muhimu katika ujenzi wa Tanzania isiyo na rushwa," alisema Ussi.Kwa upande wake, Katibu wa Klabu hiyo, Herman Paul, alisema lengo la klabu ni kuwawezesha vijana kuwa wazalendo, kutambua haki na wajibu wao, sambamba na kupambana na rushwa katika maeneo yao ya shule na jamii kwa ujumla.Klabu hiyo inaundwa na jumla ya wanachama 70, wavulana 30 na wasichana 40, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Taifa wa kuimarisha elimu ya uadilifu kwa vijana kupitia shule za sekondari.Mwenge wa Uhuru umepongeza jitihada hizo na kuahidi kuwa klabu kama hizo zitafuatiliwa kwa karibu ili kuhakikisha hazibaki kwenye nadharia bali zinakuwa sehemu ya mabadiliko chanya katika jamii.

Post a Comment