" MAAFISA MAENDELEO YA JAMII WATOA ELIMU YA FURSA ZA UCHUMI KWA WANAFUNZI WA CHUO CHA HILL FOREST SHINYANGA

MAAFISA MAENDELEO YA JAMII WATOA ELIMU YA FURSA ZA UCHUMI KWA WANAFUNZI WA CHUO CHA HILL FOREST SHINYANGA

Na Mapuli Kitina Misalaba

Maafisa maendeleo ya jamii kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga wametoa elimu ya masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi kwa wanafunzi wa Chuo cha Hill Forest Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali kuwawezesha vijana kupata uelewa wa fursa zinazowazunguka na kuzitumia kwa maendeleo yao.

Katika elimu hiyo, maafisa hao wameeleza kwa kina namna vijana wanavyoweza kujihusisha na shughuli za ujasiriamali, wakisisitiza umuhimu wa kuzingatia misingi ya kibiashara kabla ya kuanzisha biashara yoyote ili kuhakikisha inakuwa endelevu na yenye tija.

Pia, wanafunzi wamefundishwa kuhusu kuanzisha vikundi vya kiuchumi, hatua muhimu za kufuata ili kusajili vikundi hivyo, pamoja na manufaa yanayopatikana kupitia ushirikiano wa pamoja katika shughuli za kiuchumi.

Aidha, maafisa hao wamefafanua fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali, ikiwemo mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, wakibainisha kuwa fursa hizo ni nyenzo muhimu ya kuwawezesha vijana na makundi mengine kuanzisha au kukuza miradi ya kiuchumi.

Mmoja wa maafisa maendeleo ya jamii, Nyanjula Kiyenze, amesema kuwa elimu hiyo imelenga kuwajengea wanafunzi uelewa mpana wa namna wanavyoweza kujiandaa mapema kujitegemea baada ya masomo na kuepuka changamoto za ukosefu wa ajira.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Hill Forest Shinyanga, Fortunata Paschal Shine ameishukuru Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kupitia Idara ya maendeleo ya Jamii kwa kuwakumbuka wanafunzi wake na kuwapatia elimu yenye manufaa makubwa. 

Fortunata amesema kuwa elimu hiyo itawawezesha vijana kuishi kwa vitendo maarifa wanayoyapata darasani kwa kuyaunganisha na fursa za maendeleo zilizopo kwenye jamii.

Kupitia elimu hiyo, wanafunzi wa Chuo cha Hill Forest Shinyanga wametakiwa kuwa wabunifu na kujitokeza kutumia fursa zilizopo badala ya kusubiri ajira za moja kwa moja, huku wakisisitizwa kuzingatia nidhamu ya kifedha na mshikamano wa vikundi ili kufanikisha malengo yao ya kiuchumi.

Hatua hiyo ya maafisa maendeleo ya jamii inatajwa kuwa na mchango mkubwa katika kujenga mwamko wa vijana wa Shinyanga, hususan wale wanaosoma vyuoni, kwa kuwaelimisha kuhusu nafasi walizonazo kwenye mchakato wa maendeleo ya taifa na namna wanavyoweza kuwa sehemu ya mabadiliko kupitia miradi ya kiuchumi.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post