Ma Lydia Lugakila, Misalaba Media
Biharamulo
Kura za maoni za Chama cha Mapinduzi (CCM) zimeendelea kushuhudiwa Agosti 4, 2025, kama sehemu ya mchakato wa kuwapata wagombea ubunge kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Jimbo la Biharamulo Magharibi limemshuhudia Eng. Ezra John Chiwelesa akiibuka mshindi kwa kishindo kikubwa, baada ya kukusanya kura 9,215 na kuwaacha wapinzani wake mbali sana
Katika matokeo rasmi yaliyotangazwa na wasimamizi wa kura hizo, Benedict Simon Kipeja alishika nafasi ya pili kwa kura 886, huku Magnus Rutakulemberwa Banyika akipata kura 276.
Wagombea wengine ni Anatory Kasazi Choya (195), Oscar Rwegasira Mukasa (119) na Mwl. Saada Abubakari Karabaki (117).
Ushindi wa Chiwelesa umetafsiriwa na wanachama wa CCM kama ishara ya imani kubwa kwa uongozi wake na mchango wake katika maendeleo ya jamii.
Wanachama waliohudhuria kura hizo wamesema matokeo hayo ni kielelezo cha matumaini ya wananchi kuona kasi mpya ya maendeleo jimboni humo.
Kwa mujibu wa taratibu za CCM, majina ya washindi wa kura za maoni yatawasilishwa kwa vikao vya juu vya chama kwa ajili ya kupitishwa rasmi, hatua inayotarajiwa kumuweka Chiwelesa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania ubunge wa Biharamulo Magharibi kupitia tiketi ya CCM katika Uchaguzi Mkuu 2025.
Post a Comment