
Na Mapuli Kitina Misalaba
Mwenge wa Uhuru 2025 umeendelea na mbio zake ambapo
leo Agosti 6, 2025 umekimbizwa kwa jumla ya kilomita 258.5 na kumulika miradi
mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 2.8 katika
Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
Kwa kauli mbiu
isemayo "Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu
wa Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu", Mwenge wa Uhuru umefungua,
kuzindua, kukagua na kuweka mawe ya msingi kwenye jumla ya miradi 8 inayolenga
kuboresha maisha ya wananchi.
Akizungumza wakati
wa mapokezi ya mwenge huo katika eneo la, Kigwang'ona, kata ya Puni kabla ya
kuanza mbio hizo, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, amesema
kuwa Mwenge huo utakagua miradi 4, utafungua miradi 3, utazindua miradi 4 na
kuweka mawe ya msingi kwenye miradi 6, ukiwa ni sehemu ya kuchochea maendeleo
ya wananchi.
Miradi iliyomulikwa ni pamoja na:
1. Kituo
cha Mafunzo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Kata ya Didia – kilichopo katika ofisi ya maafisa ugani, mradi huu
unalenga kutoa elimu ya vitendo kwa wakulima na wafugaji.
2. Mradi
wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia – uliozinduliwa katika Shule ya Awali na Msingi Ola kwa lengo la
kulinda afya za walimu na wanafunzi dhidi ya moshi hatarishi.
3. Klabu
ya Wapinga Rushwa – imezinduliwa
katika Shule ya Sekondari Ilola ili kuimarisha maadili na kupambana na vitendo
vya rushwa miongoni mwa wanafunzi.
4. Uwezeshaji
wa Vijana Kiuchumi – kupitia
Kikundi cha Amani Ihalo ambapo vijana wamewezeshwa kupitia mkopo wa asilimia 10
kutoka mapato ya Halmashauri.
5. Mradi
wa Maji Kijiji cha Mwamakalanga, Kata ya Lyabukande – umetembelewa, kukaguliwa na kuwekwa jiwe la msingi
ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.
6. Kituo
cha Afya Lyabukande – mwenge wa
uhuru umeweka jiwe la msingi katika kituo hiki chenye umuhimu mkubwa katika
utoaji wa huduma za afya vijijini.
7. Ujenzi
wa Machinjio Ndogo ya Mifugo Kata ya Solwa – mradi huu unalenga kuboresha usafi, afya na uchumi
kupitia sekta ya mifugo.
8. Shule
ya Amali Mwambasha – inajengwa
kwa ajili ya kuwapatia vijana elimu ya ufundi na kuwawezesha kujiajiri.
Kwa upande
wake, Kiongozi
wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ali Ussi,
amesema ameridhishwa na ubora wa utekelezaji wa miradi hiyo na kupongeza
uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, hususan Mkurugenzi Dkt. Kalekwa
Kasanga kwa usimamizi makini na ubunifu mkubwa.
Ussi ameongeza
kuwa miradi hiyo inaonesha dhamira ya dhati ya serikali ya kuwaletea wananchi
maendeleo, huku akiwasisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi
mkuu 2025 kwa amani, utulivu na mshikamano.
"Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mambo makubwa
katika muda mfupi. Ni kiongozi wa mfano na wananchi wanapaswa kuendelea
kumwamini kwa ajili ya mustakabali wa taifa letu," amesema Ussi.
Mwenge wa Uhuru unaendelea na mbio zake mkoani Shinyanga ambapo kesho Agosti 7, 2025 unatarajiwa kukimbizwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, ukiendelea kuhamasisha amani, mshikamano, mapambano dhidi ya rushwa na ushiriki wa wananchi katika maendeleo ya taifa.
Post a Comment