Na Lydia Lugakila, Misalaba Media
Bukoba
Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kagera wamepatiwa mafunzo maalum juu ya matumizi sahihi ya vifaa tiba, lengo likiwa ni kuimarisha ujuzi wao katika kutumia vifaa hivyo kwa usahihi wakati wakitekeleza majukumu yao ya utoaji wa huduma.
Mafunzo hayo yameandaliwa na mkuu wa idara ya ukarabati na Matengenezo kinga, Mhandisi David Matewele, kwa kushirikiana na timu ya wataalamu kutoka idara hiyo.
Wakati wa kutoa elimu hiyo, Mhandisi Matewele alisisitiza kuwa vifaa tiba ni nyenzo muhimu katika kuokoa maisha ya wagonjwa.
Aliweka wazi umuhimu wa kuhifadhi na kutumia vifaa hivyo kwa uangalifu ili kuzuia uharibifu usio wa lazima.
“Mafunzo haya yanahusisha namna ya kutumia Sunction Mashine, njia salama za usafishaji, pamoja na utunzaji wa vifaa vinavyotumika wodini,” aliongeza.
Aidha, alitahadharisha matumizi yasiyo sahihi ya vifaa tiba yanaweza kuhatarisha huduma za afya na kuongeza gharama kubwa kwa serikali.
Ametoa wito kwa kila mtumishi kutunza vifaa vyao kwa makini na kutoa taarifa katika idara yao kuhusu hitilafu yoyote ili vifanyiwe kazi mara moja.
Watumishi waliohudhuria mafunzo hayo walipongeza menejimenti ya hospitali kwa kupanga elimu hiyo muhimu, wakieleza kuwa itawawezesha kuboresha utendaji wao wa kazi na kuchangia katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba inaendelea kujitahidi katika kuhakikisha mazingira ya kazi na huduma zinazotolewa vinakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa, ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo endelevu kwa watumishi wake katika nyanja mbalimbali za afya.
Post a Comment