Na Lydia Lugakila MbeyaMgombea Ubunge wa Jimbo la Uyole kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Tulia Ackson, amewaomba wananchi wa jimbo hilo kumchagua kwa kura nyingi pamoja na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa nafasi ya Urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025. Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa kampeni zake Septemba 13, 2025 katika Uwanja wa Shule ya Msingi Hasanga.Dkt.Tulia amesisitiza umuhimu wa kuendeleza kazi nzuri zilizofanywa katika kuboresha sekta mbalimbali za kijamii. ameeleza kuwa kati ya vipaumbele vyake ni kuhakikisha upatikanaji wa Halmashauri ya Uyole na ujenzi wa jengo lake ili kuharakisha maendeleo ya jimbo. Vipaumbele vingine vinajumuisha kuboresha miundombinu ya barabara, ujenzi wa vivuko na madaraja, kukamilisha mradi wa maji wa mto Kiwira, kuboresha huduma za afya, na kuhakikisha umeme unapatikana katika maeneo yote ya jimbo.Aidha, ameahidi kuwa ataweka mkazo kwenye maendeleo ya kilimo kwa kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo kwa wakati na kwa bei nafuu, pamoja na kuanzisha viwanja vya maonyesho na kuimarisha sekta ya michezo, hasa mchezo wa ngumi. Ufunguzi wa kampeni hizo zimehudhuriwa na wagombea wa udiwani wa kata 13 na baadhi ya wagombea wa ubunge kutoka Mkoa wa Mbeya, huku kaulimbiu ya kampeni kiwa ni "Uyole Kazi."

Post a Comment