" PICHA: CHADEMA SHINYANGA YATEMBELEA KABURI LA SHUJAA SHELEMBI KUMUENZI

PICHA: CHADEMA SHINYANGA YATEMBELEA KABURI LA SHUJAA SHELEMBI KUMUENZI

 

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Shinyanga Mjini kimeendelea kuadhimisha Wiki ya Mashujaa waliopambania chama hicho kwa lengo la kukumbuka mchango wao na kuwahamasisha wanachama wengine kuendeleza harakati za kisiasa.

Katika maadhimisho hayo, viongozi na wanachama wa CHADEMA wametembelea kaburi la  marehemu Magadula Shelembi, lililopo Kata ya Masekelo mkoani Shinyanga. Wakiwa eneo hilo wamefanya shughuli za usafi na kuomba dua kwa ajili ya kumuenzi shujaa huyo.

Akizungumza wakati wa shughuli hizo, Katibu wa CHADEMA Kanda ya Serengeti, Bw. Jackson Mnyawami, amewataka viongozi na wanachama wa chama hicho kusimama imara, kudumisha mshikamano na kuendelea kuenzi misingi iliyowekwa na mashujaa wa chama hicho, akiwemo marehemu Shelembi.

Aidha, baadhi ya viongozi na wanachama wa CHADEMA Jimbo la Shinyanga Mjini wamesema marehemu Shelembi alikuwa kiongozi jasiri, mpenda haki na mfano wa kuigwa ambaye ameacha alama kubwa katika historia ya chama hicho.

Kwa upande wake, mjane wa marehemu Shelembi, Bi. Ester Emmanuel, ametoa shukrani kwa viongozi na wanachama wa CHADEMA kwa kutenga muda wa kutembelea kaburi la mume wake na kufika nyumbani kwake kumpa faraja.

Enzi za uhai wake, marehemu Shelembi alikuwa kiongozi wa CHADEMA aliyekitumikia chama hicho katika nafasi mbalimbali.

Wiki ya Mashujaa wa CHADEMA ilianza Septemba 1, 2025, na itafikia kilele chake Septemba 7, 2025.

 

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

Post a Comment

Previous Post Next Post