" TAKUKURU MWANGA YAFANIKISHA KUREJESHWA MILIONI 24.1 SERIKALINI

TAKUKURU MWANGA YAFANIKISHA KUREJESHWA MILIONI 24.1 SERIKALINI






Na Mwandishi Wetu – Kilimanjaro

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, imefanikisha kurejeshwa zaidi ya shilingi milioni 24.1 za matibabu katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), baada ya kushinda shauri la jinai dhidi ya mtumishi wa umma.

Fedha hizo zimetokana na kesi ya jinai namba 25889/2024 iliyokuwa ikimkabili Bi. Hadija Athumani Ramadhani, mwalimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, aliyeshtakiwa kwa makosa matatu ikiwemo kughushi, kuwasilisha nyaraka zenye maelezo ya uongo na kuisababishia mamlaka hasara ya jumla ya shilingi 48,364,040/=.

Kwa mujibu wa mashitaka, Bi. Hadija alitengeneza cheti cha ndoa bandia na kumtambulisha mtu ambaye si mwenza wake halali kama mtegemezi, na hatimaye alipewa matibabu kupitia NHIF kinyume na taratibu.

Shauri hilo liliamuliwa mbele ya Mhe. Baraka Kabururu, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Wilaya ya Mwanga, ambapo upande wa mashtaka uliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Bi. Furahini Kibanga.

Bi. Kibanga aliieleza Mahakama kuwa mshitakiwa aliomba kufanya makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa njia ya Plea Bargain, ambapo alikiri makosa na kuomba shauri kumalizwa kwa maridhiano. Baada ya makubaliano hayo kukamilika, Mahakama ilimtaka mshtakiwa kukiri mashtaka yake na kutiwa hatiani.

Mnamo Septemba 18, 2025, mshtakiwa alikubali mashitaka na kusaini mkataba wa makubaliano, ambapo alihukumiwa kurejesha shilingi 24,182,020/= kwa NHIF na kupewa adhabu ya kifungo cha nje cha miezi mitatu.

Taarifa zinaonyesha tayari kiasi cha shilingi 12,091,010/= kimerejeshwa NHIF, na kilichosalia kitalipwa kwa awamu kulingana na makubaliano yaliyowekwa na Mahakama.

TAKUKURU Wilaya ya Mwanga imesisitiza kuwa haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa mtu yeyote atakayehujumu mali za umma, huku ikiwataka wananchi wote kuzingatia sheria na taratibu za matumizi ya bima ya afya ili kulinda rasilimali za taifa.

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

Post a Comment

Previous Post Next Post