Madereva wa Bajaji katika
Manispaa ya Shinyanga wamepatiwa elimu maalum ya umuhimu wa kutoa kipaumbele
kwa magari yanayobeba wagonjwa yanapokuwa yakipita barabarani, ili kuhakikisha
huduma za dharura zinawafikia wagonjwa kwa wakati.
Elimu hiyo imetolewa Askari
Polisi wa kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Shinyanga Sajenti David
Ndimila, ambaye amewaasa waendesha bajaji kutochukulia ving’ora vya magari
ya wagonjwa kama kelele za kawaida, bali kama ishara ya dharura inayohitaji
msaada wa haraka.
Sajenti Ndimila amesema kuwa
kuchelewesha magari ya wagonjwa kwa kuyazuia barabarani kunaweza kuhatarisha
maisha ya watu, hivyo ni wajibu wa kila dereva kuhakikisha anapisha njia mara
tu anaposikia ving’ora.
“Tunawaomba sana
madereva wa bajaji na vyombo vingine vya usafiri kuwa na uelewa mkubwa. Magari
haya ya wagonjwa mara nyingi hubeba watu walioko kwenye hali mbaya. Kila
sekunde ni muhimu katika kuokoa maisha yao. Tukiwapisha mapema, tunasaidia
kuokoa maisha,” amesema
Sajenti Ndimila.
Aidha, amewataka madereva hao
kufuata sheria na alama za barabarani, huku akisisitiza mshikamano na
ushirikiano kati yao na askari wa usalama barabarani ili kupunguza ajali na
kurahisisha utendaji kazi wa vyombo vya dharura.
Madereva wa bajaji waliopatiwa
elimu hiyo wameshukuru kwa mafunzo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi, huku
wakitoa wito kwa madereva wenzao wote kuhakikisha wanafuata maagizo ya usalama
barabarani kwa manufaa ya jamii.

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Post a Comment