Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga imeendelea kuboresha huduma zake kwa wananchi kwa kuanzisha na kuimarisha kitengo cha tiba za Koo, Pua na Masikio (ENT), ambacho kinalenga kuwahudumia wagonjwa wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali zinazohusiana na maeneo hayo ya mwili.
Akizungumza na Misalaba Media, mratibu wa huduma za tiba wa Hospitali hiyo, Dkt. Alistid Laudfas Ngalawa, amesema kitengo hicho ni msaada mkubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga na mikoa jirani, kwani kimekuwa kikitoa huduma za kitaalamu kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa mbalimbali ya koo, pua na masikio.
Ameongeza kuwa, kwa upande wa pua, wagonjwa wenye changamoto kama pua kuziba, kutoka makamasi mara kwa mara, areji (allergy), mafua sugu, kupungua kwa uwezo wa kunusa harufu na maumivu ya kichwa sehemu ya mbele, wanapata huduma maalumu katika hospitali hiyo.
Aidha, amesema huduma hizo pia zinahusisha wagonjwa wenye matatizo ya koo, hususan watoto wanaosumbuliwa na tontesi, kukoroma usiku, kushtuka mara kwa mara wakati wa usingizi, pamoja na watu wazima wanaopata maumivu wakati wa kumeza, kushindwa kupumua vizuri au sauti kufa.
Dkt. Ngalawa amesisitiza kuwa kwa sasa huduma hizi zinapatikana kila siku na wananchi wote wanakaribishwa kufika hospitalini hapo kwa ajili ya kupata huduma hizo muhimu.
Huduma hii ni miongoni mwa maboresho yanayoendelea kufanywa na hospitali hiyo kwa lengo la kupunguza vifo na mateso yanayosababishwa na magonjwa yanayoweza kutibika endapo yatagunduliwa mapema.
Kwa mujibu wa Mganga mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Luzila John, kuimarishwa kwa kitengo hiki kunatarajiwa kupunguza safari za wagonjwa kusafiri umbali mrefu kwenda hospitali kubwa za kitaifa, kwani sasa huduma hizi zinapatikana ndani ya Mkoa wa Shinyanga kwa gharama nafuu na huduma za kila siku.
Wananchi wote wanakaribishwa kufika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya matibabu ya koo, pua na masikio.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Post a Comment