Madereva wa pikipiki wanaojishughulisha na usafirishaji wa abiria (bodaboda) katika Manispaa ya Shinyanga wametakiwa kuheshimu misafara mbalimbali inapokuwa inapita barabarani, kwa kuzingatia maelekezo ya askari wa usalama barabarani ili kuepuka ajali na usumbufu usiokuwa wa lazima.
Wito huo umetolewa na Askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Shinyanga, Sajenti David Ndimila, wakati akitoa elimu kwa madereva hao kuhusu umuhimu wa kutii maelekezo ya mamlaka za usalama barabarani wakati wa misafara.
Sajenti Ndimila amesema baadhi ya madereva wamekuwa wakionyesha ukaidi kwa kujaribu kupita au kuzunguka maeneo yanayozuiliwa kwa muda, hali inayoweza kusababisha ajali au kuathiri usalama wa misafara husika.
Aidha, amewataka madereva wa bodaboda kujijengea utamaduni wa kuonyana na kuelimishana wao kwa wao kuhusu kutii sheria za usalama barabarani na kuacha vitendo vinavyokiuka taratibu, akisisitiza kuwa kufanya hivyo kutachangia kupunguza ajali na kuimarisha nidhamu barabarani.
Post a Comment