Na Mwandishi wetu
Tunapoadhimisha Juma la Vijana na kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, ni muhimu kurudi nyuma na kutafakari maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Hata katika enzi ya mfumo wa chama kimoja, Nyerere alisisitiza kuwa kura ni silaha ya msingi ya kila Mtanzania kuamua mustakabali wa Taifa.
Vijana wa leo, mnao wajibu wa kujitambua na kuchukua hatua. Fanyeni uchambuzi, simameni imara, na msiruhusu mtu yeyote kununua dhamira yenu.
Katika hotuba zake za kuonya Taifa, zilizojumuishwa katika mkusanyiko maarufu wa “Kilio cha Mwalimu,” Mwalimu Nyerere alitoa onyo kali dhidi ya rushwa:"Msikubali kughilibiwa kwa vizawadi vitakavyowapelekea kuuza haki zao... kuuza utu, heshima, amani na uhuru wa nchi ."
Kwa maneno mengine Baba wa taifa alijua maisha ya kila siku na kuonya vijana kwamba wasiruhusu hongo ndogo au zawadi za muda mfupi zipoteze mamlaka yako ya miaka mitano. Baba wa taifa amesisitiza katikia hotuba hizo kuwa Kura yako haina thamani ya fedha; ina thamani ya mustakabali wako kwa kuepuka siasa za migawanyiko na badala yake,kuchagua viongozi kwa msingi wa uwezo na sera zao.
Wakati wa kampeni za uchaguzi,mwaka 1975 Mwalimu Nyerere alisisitiza wajibu wa raia kutumia haki yao ya kidemokrasia: anasema "[Waliojiandikisha wanapaswa] kujitokeza kupiga kura [ili kuchagua] viongozi wanaofaa na wenye uwezo..."
Mwalimu aliona kura kama njia pekee ya kupata uongozi bora. Sasa vijana wakiwa katika mfumo wa vyama vingi, chaguo lao ni pana zaidi.
Ni kweli kuwa ikiwa Mwalimu Nyerere alisisitiza umuhimu wa kura hata wakati kulikuwa na uchaguzi wa chama kimoja tu, inamaanisha wewe kijana katika enzi hizi za utandawazi na uchaguzi wa vyama vingi,Oktoba 29, 2025: Nenda Kapige Kura! Kura yako Ndiyo Sauti Yako ya Mabadiliko!
Post a Comment