Na Lydia Lugakila, Misalaba Media
Bukoba
KAMANDA wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda, ametoa onyo kali kwa wananchi wanaokusudia kufanya vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani au kuchochea vurugu wakati wa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Bukoba, Kamanda Chatanda alisema zimebaki siku tano kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, na kwamba Jeshi la Polisi limejipanga kikamilifu kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani, utulivu na usalama wa hali ya juu.
Alisema kumekuwepo na taarifa zinazoenezwa kuwa baadhi ya wananchi wanapanga kufanya ulinzi wa kura, jambo ambalo ni kinyume cha taratibu za kisheria, kwani jukumu hilo ni la Jeshi la Polisi pekee.
Ulinzi wa kura ni jukumu la Polisi, si la mwananchi, wale wanaotaka kujichukulia jukumu hilo wajue tupo kazini.
Amesema Mpiga kura akikamilisha zoezi lake anatakiwa kuondoka eneo la kupigia kura na kurejea nyumbani kwa utulivu ili kudumisha ustaarabu,” alisema Kamanda Chatanda.
Aidha, Kamanda huyo alionya wananchi kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kusababisha vurugu au uvunjifu wa amani, akisisitiza kuwa uchaguzi ni haki ya kikatiba inayopaswa kutekelezwa kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi.
Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu yeyote atakayejihusisha na uchochezi, upotoshaji au vitendo vya uvunjifu wa amani wakati wa uchaguzi.
Tunaendelea kuwasihi wananchi wote kushiriki uchaguzi kwa amani, kuheshimu sheria na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa,” aliongeza Kamanda Chatanda.

Post a Comment