" KONGOLE RAIS DKT. SAMIA, UMEWATENDEA HAKI WAFANYAKAZI SEKTA ZOTE

KONGOLE RAIS DKT. SAMIA, UMEWATENDEA HAKI WAFANYAKAZI SEKTA ZOTE


Na: Dkt. Reubeni Lumbagala, Misalaba Media

Wafanyakazi ni kundi muhimu katika jamii na nchi hasa kutokana na umuhimu wake katika kuchagiza mabadiliko chanya na maendeleo. Wafanyakazi wa sekta zote yaani sekta ya umma (serikali) na binafsi kwa pamoja wanashirikiana katika kusimamia na kutekeleza mipango mbalimbali ya taasisi na nchi kwa ujumla ambapo kufanikikiwa kwa mipango hiyo kunachochea maendeleo na ustawi wa Taifa.

Wafanyakazi wanapaswa kutimiza majukumu yao ya kila siku kama inavyopaswa katika kuwahudumia wananchi. Waajiri wao wanawajibika kuwapa haki zao kutokana na namna wanavyotimiza majukumu yao kwa mujibu wa taratibu na miongozo ya kazi zao. Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imethibitisha si kwa maneno pekee lakini kwa vitendo kuwa ni serikali inayojali wafanyakazi kwani inathamini mchango na kazi kubwa zinazofanywa na wafanyakazi katika maendeleo ya nchi.

Moja ya eneo nyeti kwa wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi ni maboresho ya mishahara yao. Mahitaji ya nyongeza ya mishahara inatokana na uhalisia wa gharama za maisha. Kutokana na gharama za maisha, upo umuhimu wa kupitia upya viwango vya mishahara na kuviboresha hasa kwa kuzingatia mwelekeo wetu wa ukuaji wa uchumi. Rais Dkt. Samia amejipambanua kwa maneno na matendo juu ya dhamira yake ya kuboresha hali za maisha ya wafanyakazi katika maeneo kadha wa kadha, mojawapo ni nyongeza ya mishahara kwa wafanyakazi wa sekta zote yaani wa sekta ya umma na binafsi.

Mwaka 2022 akiwa na mwaka mmoja tu tangu aingie madarakani, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023, Rais Dkt. Samia aliridhia mapendekezo ya kuongeza mshahara ikiwemo kima cha chini kwa watumishi wa umma kwa asilimia 23.3. Ongezeko hilo lilipelekea serikali kutumia Shilingi 1.59 trilioni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 19.51, ukilinganisha na bajeti ya mwaka 2021/2022. Hili ni jambo kubwa sana lililofanywa na Rais Dkt. Samia kwa wafanyakazi.

Sanjari na hilo, akihutubia maelfu ya wafanyakazi Mei 1, 2025, katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Singida, Rais Dkt. Samia aliendeleza neema kwa wafanyakazi baada ya kutangaza nyongeza ya kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi wa sekta ya umma kwa asilimia 35.1. Nyongeza hii ilianza kutumika rasmi Julai 1, 2025, ambapo sasa kima cha chini kimepanda kutoka Shilingi 370,000 hadi 500,000.

"Kwa mapenzi makubwa na kwa namna mlivyoiunga mkono serikali tulipowaomba mfunge mkanda na mkaamua kujituma na kufanya kazi kwa bidii na kufanya uchumi wetu ukue kwa asilimia 5.5 mwaka huu. Kwa kuwa mcheza kwao hutunzwa mimi na wenzangu, baada ya kuangalia uchumi ulivyopanda ninayo furaha kuwatangazia kwamba, katika kuzidi kuleta ustawi kwa wafanyakazi, mwaka huu serikali itaongeza kima cha chini kwa mshahara kwa watumishi wa umma kwa asilimia 35.1," alisisitiza Rais Dkt. Samia.

Neema ya nyongeza ya mshahara haijabaki kwa wafanyakazi wa sekta ya umma pekee, neema hiyo imewashukia pia wafanyakazi wa sekta ya binafsi. Oktoba 17, 2025, serikali kupitia Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete alisema serikali imeongeza kima cha chini cha mshahara wa wafanyakazi wa sekta binafsi kutoka Shilingi 275,060 hadi 358,322 likiwa ni ongezeko la asilimia 33.4 ongezeko hili litaanza kutumika rasmi Januari 1, 2026.

Kimsingi, ongezeko hili litagusa wafanyakazi wa sekta binafsi katika sekta za hoteli, kilimo, afya, mawasiliano, usafirishaji, madini, shule binafsi, nishati,  huduma za ulinzi binafsi, utamaduni, uvuvi, biashara, viwanda, kutaja kwa uchache. "Ofisi yangu itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa amri hii, kutoa elimu kwa waajiri na wafanyakazi pamoja na kufanya tathmini ya mara kwa mara ili kuhakikisha utekelezaji wake unafanyika kikamilifu, ofisi yangu haitasita kuchukua hatua kwa waajiri watakaokaidi au kushindwa kutekeleza amri hii kwa makusudi," alisema Kikwete.

Kwa ujumla, Rais Dkt. Samia na serikali yake imefanya mengi mazuri kwa wafanyakazi wa umma na binafsi. Nyongeza ya mishahara ni sehemu mojawapo tu lakini wafanyakazi wameguswa katika maeneo mengi, mathalani, kupanda vyeo na madaraja, kulipwa madai yao ya mishahara na isiyo ya mishahara kwa wakati hasa baada ya kumalizika uhakiki wa madai yao. Kwa hakika, uboreshaji wa maslahi kwa wafanyakazi una tija kubwa hasa katika kuongeza mapato ya serikali, kuchochea mzungumo wa fedha nchini na kuchagiza ukuaji wa uchumi na maendeleo kwa ujumla.

Dkt. Reubeni Lumbagala ni mwalimu wa Shule ya Sekondari Funguni ya wilayani Pangani mkoani Tanga.

Post a Comment

Previous Post Next Post